Kipre na kocha wake mbona wapo freshi tu!

Muktasari:

Tangu kuwasili kwa Omog kikosini Azam, Tchetche amekuwa akichezeshwa nafasi ya mshambuliaji wa pembeni badala ya kucheza kati alipokuwa akipangwa wakati kikosi hicho kikinolewa na Mwingereza Stewart Hall.

MSHAMBULIAJI wa Azam, Kipre Tchetche raia wa Ivory Coast, amesema hana tatizo lolote na kocha wa timu hiyo, Joseph Omog, kwa jinsi anavyomtumia kwenye kikosi hicho. Kikubwa kwake ni timu yake kupata ushindi.

Tangu kuwasili kwa Omog kikosini Azam, Tchetche amekuwa akichezeshwa nafasi ya mshambuliaji wa pembeni badala ya kucheza kati alipokuwa akipangwa wakati kikosi hicho kikinolewa na Mwingereza Stewart Hall.

Tchetche alifanikiwa kutwaa tuzo ya Mfungaji Bora wakati akicheza straika wa kati msimu wa 2012/13.

Kuhamishwa huko kumempunguzia kasi ya upachikaji mabao, lakini yeye mwenyewe anasema kikubwa kwake ni Azam kupata ushindi kwenye mechi zake kwani ndiyo mafanikio makubwa zaidi kwake.

“Sidhani kama kuna dalili za kurejeshwa kucheza kati, sina tatizo na nafasi ya pembeni ambayo ninachezeshwa kwa sasa, nipo tayari kucheza popote ila kikubwa ni timu yangu kupata ushindi, mengine yatakuja tu,” alisema Tchetche ambaye yupo na kikosi cha timu hiyo kilichoweka kambi nchini Uganda.

“Usajili uliofanyika sidhani kama utabadilisha nafasi yangu kwenye kikosi, ila waliokuja ni wachezaji wazuri, natumai wataisaidia timu kwani hadi kusajiliwa Azam inamaanisha kuwa wana uwezo mzuri uwanjani,” aliongeza mchezaji bora huyo wa msimu uliopita.

Tangu Tchetche alipojiunga na Azam miaka mitatu iliyopita, amekuwa na mafanikio makubwa na kufanikiwa kuisaidia timu hiyo kunyakuwa taji la kwanza la Ligi Kuu Bara msimu uliopita huku yeye akitwaa tuzo ya Mfungaji Bora mara moja na Mchezaji Bora mara mbili.

Ni Mchezaji Bora wa msimu uliopita na Mchezaji Bora wa Kigeni mwaka 2014.