Kinachomsumbua Kaseke hiki hapa

Muktasari:

Kaseke alikuwa hakosekani katika kikosi cha kwanza enzi za kocha mzungu, Hans Van Pluijm lakini maisha yake yamebadilika gafla na kujikuta akipoteza nafasi chini ya kocha Mzambia, George Lwandamina.

NYOTA wa Yanga, Deus Kaseke amejikuta katika wakati mgumu klabuni hapo baada ya kupoteza nafasi ya katika kikosi cha kwanza huku akikabiliwa na ushindani mkubwa wa kuwa chaguo la pili pia.

Kaseke alikuwa hakosekani katika kikosi cha kwanza enzi za kocha mzungu, Hans Van Pluijm lakini maisha yake yamebadilika gafla na kujikuta akipoteza nafasi chini ya kocha Mzambia, George Lwandamina.

Nyota wa zamani wa Yanga, Aaron Nyanda amefichua kwamba kinachomkwamisha nyota huyo ni kukosa umakini katika eneo la mwisho ambapo amekuwa akipoteza nafasi nyingi ambazo angeweza kufunga.

Nyanda alisema Lwandamina anapendelea mchezaji mwenye akili ya kushambulia lakini Kaseke amekuwa imara zaidi katika kukaba lakini siyo mzuri katika kushambulia hivyo kama anataka kupata nafasi ni lazima ajitathmini upya.

“Kaseke anacheza vizuri katika kukaba lakini ana mapungufu katika kushambulia. Pasi zake za kupenyeza siyo nzuri na amekuwa akipoteza nafasi nyingi. Nadhani kocha anapendelea mtu ambaye ana kasi na anakwenda mbele zaidi,” alisema Nyanda.