Kina Mwanjali na Chirwa wanatufundisha kitu

Muktasari:

Katibu wa Baraza la Wazee, Ibrahim Akilimali alimkosoa mchezaji huyo katika mchezo wake wa kwanza tu wa Kombe la Shirikisho dhidi ya TP Mazembe ya DR Congo Uwanja wa Taifa akisema kwamba si lolote wala si chochote.

OBREY Chirwa ni miongoni mwa wachezaji wa kigeni wa Yanga waliokosolewa zaidi ndani ya Yanga tangu msimu huu uanze. Alikosolewa na wanachama na mashabiki kwa madai kwamba bei iliyotangaziwa ya manunuzi yake pamoja na mshahara wake anaipoewa pale Jangwani haviendani na ufanisi wake wa uwanjani.

Katibu wa Baraza la Wazee, Ibrahim Akilimali alimkosoa mchezaji huyo katika mchezo wake wa kwanza tu wa Kombe la Shirikisho dhidi ya TP Mazembe ya DR Congo Uwanja wa Taifa akisema kwamba si lolote wala si chochote.

Lakini ghafla mchezaji huyo ameanza kuonyesha uwezo wake na kuwaziba midomo wakoseaji wake na kuwafanya wanywee mmoja baada ya mwingine baada ya kurudi kwenye fomu yake ya ufungaji wa mabao manane sawa na Donald Ngoma ambaye wako naye wa Yanga na John Bocco wa Azam.

Kinachomtokea Chirwa kilianza kunukia pia kwa Mzimbabwe wa Simba, Method Mwanjali lakini akachukua muda mfupi sana kuwathibitishia, wanachama na mashabiki wa Simba kwamba hawakufanya makosa kumsajili.

Mwanjali pamoja na umri wake kumtupa lakini amekuwa tegemeo kubwa ndani ya kikosi cha kwanza mpaka sasa na kama akikosena katika mchezo wowote ule, Simba huingiwa na wasiwasi. Simba sasa hawana maneno kabisa na Mwanjali na anaaminiwa kama waziri wa ulinzi katika safu ya ulinzi ya timu hiyo.

Wachezaji hao ni mfano tu wa wachezaji wa kigeni ambao walikumbana na changamoto na usajili wao ukakosolewa kwa namna moja au nyingine kutokana na timu zetu za Simba na Yanga kutokuwa na subira au uelewa wa mambo. Lakini maoni yetu ni kwamba kuna utaratibu wa maana zaidi unaoweza kufanyika na klabu zenye uwezo wa kifedha wa kusajili wachezaji wa kigeni zikapata wachezaji wa maana zaidi ya hao waliopo sasa.

Kwavile ukijaribu kuangalia karibu wachezaji wote walionunuliwa wana umri mkubwa ambao unaashiria kwamba soka lao limefikia ukingoni na kwamba hawawezi kucheza soka jingine lenye ushindani zaidi ya huu wa Tanzania Bara.

Tunazisisitiza klabu zitumie muda wao na wataalamu kusaka wachezaji wa maana zaidi nje ya mipaka ya Tanzania ambao wanaweza kuleta ushindani wa kweli na kuboresha ligi yetu, tusing’ang’anie wachezaji wa fasheni au majina ya nchi.

Matokeo ya kufanya usajili wa zimamoto ndio unazifanya klabu kuibuka na maveterani lakini wakitumia muda wao kufanya kazi na kufuatilia wachezaji kwa muda mrefu watapata watu wa maana. Klabu zitumie mawakala na mabenchi yao ya ufundi kusaka wachezaji wa maana. Tujaribu kujiuliza kama mchezaji mwenye miaka 38 au 40 pale Zimbabwe, Zambia au Ghana anaweza kuonyesha ushindani kama ilivyo sasa, itakuwaje kama wakipatikana wenye umri mdogo zaidi na wenye damu zinazochemka na ambao wanachezea timu zao za taifa?

Kama tumeamua kuwekeza na kusaka mafanikio tufanye kweli, kwavile gharama zinazotokana na wachezaji wa kigeni ni kubwa sana hivyo lazima zitumike kikamilifu na wapatikane watu wanaojua kazi kweli.

Tuache kufanya mambo kwa mazoea tufanye kazi inayoendana na hadhi ya soka letu.

Uwepo wa wachezaji wa maana wa kigeni utasaidia kuitangaza ligi yetu kwavile, kwanza uwezekano wa kuwauza kwenye ligi za maana upo kwavile ligi yetu inaonyeshwa na inaonekana mbali kwa sasa na mawakala kibao wanavutiwa nayo.

Kuuza wachezaji kwenye ligi za nje husaidia pia kuitangaza ligi husika pamoja na jina la nchi na inaongeza mvuto kwa watu kutaka kujihusisha nayo zaidi.

Lakini tofauti na hivyo, kwa sasa tumeifanya ligi yetu kuwa kimbilio la wakongwe ambao umri umeshawatupa. Hali hiyo haiwezi kuifanya ligi yetu ijulikane duniani.

Tubadilike tuumize kichwa kupata wachezaji bora zaidi.