Kikosi ghali cha Ligi Kuu England

Wednesday May 17 2017

 

By Mwanasporti

        DIRISHA la usajili wa majira ya kiangazi mwaka jana lilishuhudia pesa kibao zikitoka na kufikia hatua ya kuvunja rekodi ya dunia kwenye uhamisho.

Klabu za Ligi Kuu England zilifanya matumizi makubwa huku Paul Pogba, aliyetua Manchester United kutoka Juventus akiweka rekodi ya dunia ya kuwa mchezaji ghali zaidi.

Lakini, wakati bingwa wa Ligi Kuu England msimu huu akiwa ameshapatikana, Chelsea, huku ligi yenyewe ikitarajia kufika tamati Jumapili, hiki hapa ni kikosi cha kwanza cha wachezaji ghali zaidi kwenye ligi hiyo msimu huu.

KIPA: CLAUDIO BRAVO (MAN CITY, PAUNI 17 MILIONI)

Kwa kifupi, Claudio Bravo, ni majanga tu kwenye kikosi cha Manchester City. Kocha Pep Guardiola alitoa pesa nyingi kuipata sahihi yake akiamini atakuwa msaada, lakini msimu wake wa kwanza umeonekana kuwa mgumu.

Baada ya mambo kuzidi kuwa mabaya, kocha Guardiola aliamua kubadili mawazo yake na kuanza kumtumia kipa Willy Caballero kuwa chaguo lake namba moja, lakini jambo hilo halimfanyi Bravo kuondoka kwenye orodha ya wachezaji walionaswa kwa pesa nyingi kwa msimu huu na ndiye kipa wa kikosi ghali cha Ligi Kuu England msimu huu.

BEKI WA KUSHOTO: MARCOS ALONSO (CHELSEA, PAUNI 24 MILIONI)

Kama kuna wachezaji ambao kocha Antonio Conte anafurahi kuwa nao katika kikosi cha Chelsea, basi mmoja wao ni Marcos Alonso.

Beki huyo wa zamani wa Bolton Wanderers, ameonyesha kiwango kikubwa tangu alipotua Chelsea na mchango wake umeisaidia timu hiyo kubeba taji la Ligi Kuu England msimu huu.

Kwenye ule mfumo wa 3-4-3 ulioanzishwa na Conte kwenye kikosi hicho, Alonso ameonyesha kiwango kikubwa na anahusika kwa kiasi kikubwa katika mafanikio ya timu hiyo ya Stamford Bridge.

BEKI WA KATI: ERIC BAILLY (MAN UNITED, PAUNI 32 MILIONI)

Ni beki mtulivu kutoka Ivory Coast na anatajwa kuwa ni moja ya usajili bora kabisa uliofanywa na Jose Mourinho kwenye kikosi cha Manchester United kwa msimu huu. Huduma ya Bailly haina mashaka na anaaminika atakuwa kisiki cha maana zaidi katika beki ya Man United kwa siku zijazo hasa kutokana na umri wake ukiwa bado unaruhusu. Tatizo la kuwa majeruhi lilimtibulia na kujikuta akicheza mechi 23 tu za Ligi Kuu England msimu huu.

BEKI WA KATI: JOHN STONES (MAN CITY, PAUNI 47.5 MILIONI)

Mwanzoni alipotua kwenye kikosi cha Manchester City wengi walikosoa ada yake ya uhamisho iliyolipwa kumpata, walisema pesa iliyolipwa ni nyingi kuliko uwezo wake.

Mwanzoni kiwango cha soka lake kilimfanya asionekane kabisa kuwa beki wa kusajiliwa kwa ada inayokaribia Pauni 50 milioni. Lakini, katika duru la pili la msimu, John Stones, alitulia ndani ya uwanja na alionekana kuelewa vizuri falsafa za kocha Pep Guardiola anayehitaji zaidi soka la kupiga pasi na hakika msimu ujao kuna kitu kizuri zaidi kinatarajiwa kutoka kwake.

BEKI WA KATI: SHKODRAN MUSTAFI (ARSENAL, PAUNI 35 MILIONI)

Sahihi yake kuipata kwa Pauni 35 milioni ilionekana kama ni pesa kidogo kutokana na kiwango chake alichokionyesha uwanjani na kufananishwa na Nemanja Vidic.

Mustafi anakuwa beki ghali katika historia ya Arsenal na hakika mchango wake umeonekana bayana kwani anapokosekana tu katika kikosi cha kwanza, pengo lake linaonekana bila kificho.

Kwenye mfumo wa kutumia mabeki watatu, Mustafi ni mchezaji anayeweza kufiti vizuri na kumpa kocha uhakika wa ulinzi wa kiwango cha juu.

BEKI WA KULIA: JORDON IBE (BOURNEMOUTH, PAUNI 15 MILIONI)

Kwenye kikosi hiki cha wachezaji ghali zaidi, Jordon Ibe, anatumika nafasi ya beki wa kushoto anayepanda kushambulia. Huyu ndiye mchezaji aliyesajiliwa kwa pesa nyingi sana katika klabu ya Bournemouth wakati aliponaswa kutoka Liverpool. Hata hivyo, kiwango chake kwa msimu huu kimekuwa cha kupanda na kushuka matokeo yake amejikuta akianzishwa kwenye mechi 13 tu za Ligi Kuu England. Kwenye mkataba wake, Liverpool wameweka kipengele cha kumnunua tena kama ataonyesha makali ya juu.

KIUNGO WA KATI: PAUL POGBA (MAN UNITED, PAUNI 89 MILIONI)

Ndiye mwanasoka ghali zaidi duniani kwa sasa. Mwanzoni mwa msimu, Paul Pogba, alionekana kupata shida kidogo na kuwafanya watu kudhani kwamba anacheza huku akiwa anasumbuliwa na ada ya uhamisho iliyolipwa kwenye uhamisho wake. Lakini, baadaye, Pogba alionyesha kiwango kizuri kabisa katika kikosi chake cha Man United na matumaini ni makubwa kabisa kwamba msimu ujao atakuwa moto kweli kweli.

KIUNGO WA KATI: GRANIT XHAKA (ARSENAL, PAUNI 35 MILIONI)

Aliponaswa ilidhaniwa kwamba Arsenal imepata suluhisho la kudumu kuhusu tatizo lake la kiungo wa kati lililokuwa likiisumbua, lakini staa huyo wa kimataifa wa Uswisi soka lake la kutumia nguvu limemfanya ajikute akiishia kuonyeshwa kadi nyekundu tu za mara kwa mara kwenye Ligi Kuu England.

Xhaka bado ameweza kuonyesha ubora wake katika kutoa mchango wa kuisaidia Arsenal kufanya vizuri katika baadhi ya mechi na kuvuna matokeo mazuri.

KIUNGO WA KUSHOTO: LEROY SANE (MAN CITY, PAUNI 42 MILIONI)

Ilihitaji muda kidogo kwa kiungo huyo wa kushoto, Leroy Sane, kutuliza daruga zake klabuni Manchester City huku akiwa ni usajili wa pesa nyingi katika kikosi hicho wakati aliponaswa kutoka Hamburg.

Lakini, hadi alipofika Desemba alianza kuonyesha uwezo wake ndani ya uwanja na kuwapa shida mabeki wa timu pinzani. Mjerumani huyo ni miongoni mwa wachezaji waliosajiliwa kwa pesa nyingi na wamefanya vizuri kwenye Ligi Kuu England.

KIUNGO WA KULIA: SADIO MANE (LIVERPOOL, PAUNI 34 MILIONI)

Liverpool iliinasa sahihi ya Msenegali huyo kwa Pauni 34 milioni akitokea Southampton. Sadio Mane alionyesha thamani halisi ya pesa yake kutokana na kufanya vizuri katika kikosi cha Liverpool akiwa amefunga mabao 13 na kuasisti mengine, huku akifanikiwa kuchaguliwa kuwa Mchezaji Bora wa Mwaka wa Liverpool. Kwenye kikosi hiki cha wachezaji waliosajiliwa kwa pesa nyingi kwenye Ligi Kuu England msimu huu, Mane anacheza kiungo wa kulia.

STRAIKA: MICHY BATSHUAYI (CHELSEA, PAUNI 33 MILIONI)

Katika msimu wake huu wa kwanza, Michy Batshuayi, amekuwa maarufu zaidi kwenye mitandao kuliko hata uwanjani hadi hapo alipofunga bao lililoifanya Chelsea kubeba ubingwa wa Ligi Kuu England msimu huu Ijumaa iliyopita kwenye mechi dhidi ya West Brom. Batshuayi alisajiliwa kwa pesa nyingi ikidhaniwa atakuja kuwa tishio kwenye kikosi hicho kumpa wakati mgumu Diego Costa, lakini mambo yamekuwa tofauti kabisa.