Kiherehere cha Yanga chaitoa Simba mjini

Mashabiki wa Yanga waliojitokeza Uwanja wa Ndege wa JNIA wakiishangilia timu yao baada ya kutua na taji hilo kutoka Mwanza. Picha na Ericky Boniphace

Muktasari:

Hata hivyo, sasa makelele ya Yanga ambayo ilitua Dar es Salam jana mchana wakitamba na kombe hilo kwenye barabarani mbalimbali pamoja na kutoa maneno ya kejeli, yamewachefua Simba ambao leo Jumatatu watalikimbia jiji kwa muda kujificha Morogoro

SIMBA imeonyesha stakabadhi  ambazo zimethibitisha kwamba kuna mzigo wametuma Fifa na si tu kwamba umewasili, bali umeshapokelewa.

Mnyama anasisitiza amekata rufaa Fifa wakitaka kurudishiwa pointi tatu za Kagera Sugar ambazo walipokwa na TFF.

Simba wanasisitiza, wao bado wana nafasi ya kuwa bingwa wakipewa pointi hizo na ndio maana walisusia medali za nafasi ya pili baada ya kuifunga Mwadui juzi Jumamosi na wakashangaa kwanini TFF waliwapa Yanga kombe kule Mwanza.

Hata hivyo, sasa makelele ya Yanga ambayo ilitua Dar es Salam jana mchana wakitamba na kombe hilo kwenye barabarani mbalimbali pamoja na kutoa maneno ya kejeli, yamewachefua Simba ambao leo Jumatatu watalikimbia jiji kwa muda kujificha Morogoro huku wakiendelea kuiwazia Mbao FC.

Simba wanakimbilia nyodo za Yanga, lakini wanakwenda kuipigia hesabu Mbao ambao iliwanyoosha Yanga kwa mara ya pili Jumapili jijini Mwanza kwa kipigo cha bao 1-0 na kutibua utamu wa sherehe zilizofanyika kwenye ukumbi wa Villa Park.

Simba na Mbao zinakutana kwenye fainali ya Kombe la FA Jumamosi ijayo mjini Dodoma, ambapo bingwa wa mchezo huo ataiwakilisha nchi kwenye Kombe la Shirikisho na kama Fifa hawatatamka kitu Yanga itakwenda Ligi ya Mabingwa Afrika ambako tayari Al Ahly wanawasubiri kwa hamu.

Simba inaonekana kuwa na hofu kubwa kukutana na Mbao kutokana na ugumu  wa kupata ushindi kwenye mechi zao za ligi ingawa mechi zote Simba walishinda, mechi ya kwanza iliyochezwa Uwanja wa Uhuru, Simba ilishinda bao 1-0 wakati mechi ya marudiano iliyochezwa CCM Kirumba, Simba walishinda bao 3-2 kwa mbinde kwelikweli.

Mbao imewafanya Simba walione jiji la Dar es Salaam la moto kutokana na kumbukumbu ya kupata matokeo ya jioni wanapocheza nao kwani, wanakutana na upinzani mkubwa na ndiyo maana leo Jumatatu wanakwenda Morogoro kupiga kambi kwa maandalizi.

Habari kutoka ndani ya Simba zinasema kikosi hicho kitakuwepo mjini Morogoro kama hakutakuwa na mabadiliko yoyote ambapo, Alhamisi wataanza safari ya kwenda Dodoma ambako ni mwendo wa saa takribani tatu hivi.

Jamhuri pako safi

Kwa mujibu wa Chama cha Soka Dodoma (Dorefa) timu zitawasili muda wote kuanzia leo Jumatatu, lakini uwanja umeboreshwa kila sehemu ndani na nje hususani sehemu ya kuchezea ambapo kwa sasa haukauki maji na ulinzi kwenye uwanja huo ni wa hali ya juu.

Meneja wa uwanja huo, Anthony Nyembera amesema lengo ni kuona timu zote mbili zikicheza vyema na kusiwepo na lama wala visingizo vya uwanja chakavu iwapo mmoja atagongwa na kulikosa kombe hilo.

Nyembera aliongeza kuwa siku tano zilizobaki wanaweka uzio maalum kuzunguka sehemu ya ndani ya uwanja huo ili nyasi zisiguswe na mtu zaidi ya maji pekee kabla ya siku ya mwisho ambayo wataufungua kwa ajili ya timu hizo kuutumia kwa mazoezi ya mwisho kabla ya fainali hiyo inayosubiriwa kwa hamu kubwa na mashabiki wa soka wa Dodoma.

“Lengo letu ni kuona uwanja unakuwa kwenye ubora unaotakiwa na imani yetu kabla ya Jumamosi uwanja utakuwa safi kutumika kwa mchezo huo wa fainali na ili kufanikisha hilo tutaweka ulinzi maalum kuzunguka uwanja ili mtu asikanyage nyasi kabisa,” alisema.