Kichuya hajafulia, nyie subirini muone

Friday January 6 2017SHIZA KICHUYA

SHIZA KICHUYA 

By THOMAS NG’ITU

WINGA machachari wa Simba, Shiza Kichufa hajafunga bao lolote tangu duru la pili lianze, kiasi cha kumfanya afikiwe na washambuliaji wenzake wa timu pinzani Simon Msuva na Amissi Tambwe, lakini mwenyewe wala hajashtuka.

Kichuya amedai amewasikia wale wote wanaomponda na kudai amefulia kwa sasa kwamba wajiandae kuaibika kwani anarejea kwenye kasi yake ya kufunga kuonyesha kuwa hakubahatisha kwenye duru la kwanza.

Mara ya mwisho kwa Kichuya kufunga ni Novemba 2 mwaka jana wakati Simba ikishinda bao 1-0 dhidi ya Mwadui, akilifunga kwa penalti, lakini ameliambia Mwanaspoti kuwa hajakata tamaa kwani anajua atafunga tu akipata nafasi.

Alisema kwanza yeye si mshambuliaji anayepaswa kufunga mara kwa mara, lakini kwa kuwa ana kipaji nafasi ikipatikana hafanyi ajizi, huku akisisitiza anafurahi kuona anaisaidia Simba kupata matokeo mazuri uwanjani.

“Unajua katika soka ukiona mtu anafunga inabidi watambue kuwa ni muda wake alioandikiwa na Mungu afunge, hata uwe unataka kufunga vipi na kujitutumua lakini kama haijaandikwa ufunge huwezi kufunga”, alisema.