Kerr aifitinisha CAF kwa Yanga

DYLAN KERR

Muktasari:

  • Yanga ndiyo timu pekee ambayo haikupumzika wakati ligi kuu ilipomalizika Mei mwaka huu, ilikuwa ikishiriki hatua ya makundi Kombe la Shirikisho Afrika kufuatia kung’olewa kwenye Ligi ya Mabingwa iliyokuwa ikishiriki awali.

KOCHA Dylan Kerr alitimuliwa na Simba Januari mwaka huu baada ya kupoteza Kombe la Mapinduzi, lakini licha ya kuwa mbali na Bongo bado amekuwa akifuatilia Ligi Kuu Bara na jana Alhamisi aliibuka na jambo ambalo Yanga ni lazima wavimbe midomo kuinunia Caf (Shirikisho la Soka Afrika).

Kocha huyo raia wa Uingereza, alifichua siri kwamba pamoja na Yanga kuwa na kikosi bora itaingia katika mchezo wa watani wa jadi Oktoba Mosi ikiwa na hasara ya uchovu wa mashindano wa kimataifa yanayosimamiwa na Caf.

Yanga ndiyo timu pekee ambayo haikupumzika wakati ligi kuu ilipomalizika Mei mwaka huu, ilikuwa ikishiriki hatua ya makundi Kombe la Shirikisho Afrika kufuatia kung’olewa kwenye Ligi ya Mabingwa iliyokuwa ikishiriki awali.

Kerr alisema Yanga imecheza mechi nyingi mwaka huu hivyo wachezaji wake hawana kiu na mpira kama ilivyo kwa Simba ambayo imeanza msimu kwa kasi na kuongoza ligi hiyo mpaka sasa ikiwa ndio kwanza ipo raundi ya tano tu.

“Yanga inaingia katika mchezo wa watani wa jadi ikiwa imechoka kiasi, unajua mwaka huu hawajapumzika hivyo inaweza kuwa changamoto kwao,” alisema Kocha Kerr.

“Simba naona wameanza msimu vizuri, hii inamaanisha wataingia katika mchezo huo wakiwa moto, pengine hili linaweza kuwabeba,” alifafanua.

Hata hivyo kocha huyo alidai kuwa ushindi mfululizo wa Simba ikicheza nyumbani hauwezi kutoa taswira ya ubingwa kwani bado wana kazi ngumu katika viwanja vya ugenini ambavyo ndiyo huamua bingwa wa Ligi Kuu Bara.

Ikiwa chini yake Simba katika mchezo wa kwanza wa msimu uliopita ilipigwa mabao 2-0 na alipotimuliwa na nafasi yake kuchukuliwa na msaizidi wake, Jackson Mayanja iligongwa tena mabao 2-0 na kuibua misemo ya Wa Mchangani na Matopeni kwao.