Kavumbagu yupo zake Kariakoo

Straika  Mrundi Didier Kavumbagu.

Muktasari:

  • Kavumbagu aliichezea Yanga miaka ya nyuma akahamia Azam FC aliyoichezea hadi msimu uliopita, lakini hawakumwongezea makataba mpya, akaamua kwenda nchi Vietnam kusaka timu.

STRAIKA Mrundi Didier Kavumbagu hajasajiliwa na klabu yoyote Bongo, lakini baada ya michakato yake ya kupata timu kugoma, ameamua kubaki nchini akikatiza mitaa ya Kariakoo na kujifua katika fukwe za Bahari ya Hindi maeneo ya Mikocheni jijini Dar es Salam.

Kavumbagu aliichezea Yanga miaka ya nyuma akahamia Azam FC aliyoichezea hadi msimu uliopita, lakini hawakumwongezea makataba mpya, akaamua kwenda nchi Vietnam kusaka timu.

Lakini akiwa huko, alikumbana na tatizo, aligundulika amesaini katika klabu mbili tofauti akakosa sifa, ndipo akaamua kurudi Tanzania na kuweka kambi ya maandalizi mengine.

Kavumbagu ambaye alikuwa anaishi na familia yake nchini na sasa ameirudisha kwao Burundi alisema: “Bado niponipo hapa Bongo nikishughulikia mipango mingine ya kucheza baada ya kupata matatizo Vietnam. Kule kulitokea mchanganyo katika mambo ya mkataba ikawa bahati mbaya nikashindwa kucheza.”

“Ndipo nikaamua kurudi Tanzania nijipange na kufanya maandalizi mengine na sasa nafanya mambo yangu huku najifua ufukweni mwa bahari kule Mikocheni karibu na Escape one, mambo yakienda sawa naondoka,”alisema Kavumbagu.