Kapuya atia neno usajili Simba

Muktasari:

Akizungumza na Mwanaspoti, Profesa Kapuya alisema Simba wapo vizuri sana nafasi ya viungo na ulinzi, lakini hawana washambuliaji makini ambao wanaweza kuipa magoli mengi hivyo, ni lazima safu hiyo iimarishwe.

ALIYEKUWA mbunge wa Urambo Mashariki na mwanachama wa kulia wa Simba, Profesa Juma Kapuya amewataka viongozi wa klabu hiyo kufanya usajili wa maana msimu ujao pamoja na ushiriki wao katika michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika. Amewataka viongozi wa Simba kuhakikisha wanasajili  mastraika wawili wa maana ili kunoa makali ya safu ya ushambuliaji.

Akizungumza na Mwanaspoti, Profesa Kapuya alisema Simba wapo vizuri sana nafasi ya viungo na ulinzi, lakini hawana washambuliaji makini ambao wanaweza kuipa magoli mengi hivyo, ni lazima safu hiyo iimarishwe.

“Mechi ilikuwa ngumu, Mbao hawajaingia kwenye fainali kwa kubahatisha ni timu ambayo inapambana kuhakikisha inashinda, kutokana na ushindani uliokuwepo haikuwa rahisi kutabiri nani ataibuka mshindi, lakini mwenye bahati ndiye angekuwa mshindi hivyo katika mechi hii Simba ilikuwa na bahati ya kushinda.

“Simba sasa wanatakiwa kutulia kufanya usajili wao ila waimarishe zaidi nafasi pale mbele, wasajili hata wawili ambao watakuwa bora katika timu yaani waje Simba kuchezana sio kukaa benchi,” alisema Kapuya.

Tayari Simba imemnasa straika wa Azam FC, John Bocco ambaye inadaiwa anaweza kuchukuwa nafasi ya Ibrahim Ajibu, ambaye mkataba wake umemalizika na inadaiwa hataki kusaini mpya kwani ana mpango wa kutimka.

Ajibu ni miongoni mwa wachezaji wanaotajwa kuwaniwa na Yanga pamoja na Singida United iliyopanda daraja kucheza Ligi Kuu Bara msimu ujao.