Kamati ya saa 72 kwa masilahi ya nani?

Muktasari:

Saanya aliboronga kwenye mechi ya Simba na Yanga iliyomalizika kwa sare ya bao 1-1, kila mmoja alipiga kelele kutokana na uchezeshaji mbovu wa mwamuzi huyo na suala lake lilianza kushughulikiwa mara moja na uamuzi wa awali ulikuwa wa kumfungia miaka miwili ila baada ya taarifa hizo kuvuja, waliamua kufuta na kwamba wapo kwenye uchunguzi huku wakifuta adhabu ya kadi nyekundu ya Jonas Mkude aliyopewa na Saanya.

MBONA ishu ya Martin Saanya ilikuwa ‘fasta’ tu? Unaweza kujiuliza hivyo baada ya Kamati ya Saa 72 kushindwa kutoa uamuzi wake kwenye vurugu zilizojitokeza mechi ya Ligi Daraja la Kwanza (FDL) kati ya Coastal Union na KMC zilizopelekea mwamuzi Thomas Mkombozi kushambuliwa kwa mawe na mashabiki wanaodaiwa kuwa ni wa Coastal Union huku mwamuzi huyo akifunguka ilivyokuwa.

Saanya aliboronga kwenye mechi ya Simba na Yanga iliyomalizika kwa sare ya bao 1-1, kila mmoja alipiga kelele kutokana na uchezeshaji mbovu wa mwamuzi huyo na suala lake lilianza kushughulikiwa mara moja na uamuzi wa awali ulikuwa wa kumfungia miaka miwili ila baada ya taarifa hizo kuvuja, waliamua kufuta na kwamba wapo kwenye uchunguzi huku wakifuta adhabu ya kadi nyekundu ya Jonas Mkude aliyopewa na Saanya.

Wiki iliyopita, Mwamuzi Thomas Mkombozi alichezea kipigo kutoka kwa mashabiki kilichompelekea kulazwa hospitali kwa muda baada ya kulalamikiwa kuwa alitoa penalti isiyokuwa halali kwa KMC ilipocheza na Coastal United kwenye Uwanja wa Mkwakwani, Tanga.

Mjumbe wa Kamati ya Saa 72, ambaye pia ni Mkurugenzi wa Bodi ya Ligi, Boniface Wambura alisema haijulikani kamati hiyo itakutana lini kwani wanakusanya taarifa zaidi.

Mjumbe wa Kamati ya Chama Waamuzi Tanzania (FRAT), Kanali Isalo Chacha alisema: “Mwamuzi ni binadamu kama binadamu mwingine, ana mapungufu yake. Kitendo cha kumpiga mwamuzi hakikubaliki hata kama amechezesha vibaya, walipaswa waandike malalamiko yao ili yakasikilizwe na si kumpiga, hata TFF kupitia kamati yao hiyo kuchelewa kuchukua uamuzi kwa mambo ambayo ni ya wazi watasababisha maafa makubwa.”

“Katika tukio hilo sioni kama kulikuwa na sababu ya kukaa kimya mpaka wakati huu, wachukue hatua.”

 

MKOMBOZI AFUNGUKA

Mwamuzi Mkombozi ambaye ni afande alisema: “Mashabiki wanatakiwa kutambua kuwa kuna kushinda na kushindwa kama mwenyeji hapendi kufungwa basi hakuna haja ya kucheza nyumbani na ugenini. Nashukuru nilijitahidi kupambana kupangua virungu, mawe yaliyokuwa yakirushwa maana ilikuwa hatari sana, niliumizwa kidogo kichwani na maumivu makali yaliyotokana na kurushiwa mawe ndiyo yaliyopelekea nilazwe, sasa hivi nimerudi kwangu Moshi.”

 

MAKOCHA WANENA

Kocha Msaidizi wa Stand United, Athman Bilali ‘Bilo’ alisema kuwa: “FDL kule hakuna sheria, mauaji yanaweza kutokea wakati wowote wachezaji wenyewe huwezi hata kuchagua nani mchezaji bora wa mechi, maana ni vurugu tupu, waamuzi ndiyo kabisa maana hakuna anayefuatilia. TFF na Bodi ya Ligi wanapaswa kuangalia zaidi FDL maana ndiko kwenye mzizi wa wachezaji bora wa ligi kuu. Kiungwana mwamuzi Mkombozi hajatendewa haki, huo ni mpira wa kizamani kumpiga mwamuzi. TFF wasikae kimya kwa muda wote huu,” alisema Bilo.

Jackson Mayanja ambaye ni Kocha Msaidizi wa Simba naye alisema: “Mwamuzi ni binadamu kama binadamu mwingine, kila mmoja afanye kazi yake kwa nafasi yake, tukisema tuwe tunawakataa waamuzi tutachezeshwa na nani, kikubwa wazingatie kanuni na sheria za soka.”