Kama zali Yanga yarudishwa Taifa

KLABU ya Yanga imepiga bao, baada ya jana Ijumaa kuingia mkataba na Serikali ili kuutumia tena Uwanja wa Taifa pamoja na Uhuru vilivyopo jijini Dar es Salaam kwa michezo yao ya Ligi Kuu Bara na ile ya kimataifa.

Yanga ilizuiwa kuutumia Uwanja wa Taifa na kuhamia Uhuru tangu baada ya pambano lao dhidi ya Simba kutokana na uharibifu uliotokea uwanjani hapo Oktoba Mosi mwaka huu ambapo timu hizo zilitoka sare ya bao 1-1.

Katibu Mkuu wa Yanga, Baraka Deusdedit alilithibitishia Mwanaspoti jana Ijumaa mchana kuwa, wamesaini mkataba huo na Katibu Mkuu Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Prof. Elisante Ole Gabriel kwa niaba ya serikali.

Kwenye mkataba huo Yanga imeruhusiwa kutumia viwanja hivyo kama viwanja vyake vya nyumbani kwa sharti la kuvitunza wakati wote wanapovitumia.

Hatua ya Yanga kurudi serikalini imetokana na kubanwa na kanuni mpya za Shirikisho la Soka la Afrika (Caf) juu ya Leseni za Klabu inayotaka timu kuwa na uwanja wa mazoezi na wa mechi na Deusdedit alisema sasa wameruhusiwa kutumia viwanja hivyo kwa mazoezi pamoja na mechi.

“Tumesaini mkataba na serikali juu ya Yanga kuutumia Uwanja wa Taifa na Uhuru kwa mechi za kimataifa na kitaifa na tumepewa masharti ambayo ni lazima tutekeleze,” alisema Deusdedit.

Moja ya masharti waliyopewa Yanga ni kutunza viwanja, mali na vifaa vyote vilivyopo uwanjani hapo na endapo kutatokea uharibifu wowote utakaofanywa na wachezaji au mashabiki Yanga itawajibika kubeba mzigo wote.