Kama unataka ubingwa mnunue Tambwe

STRAIKA Amissi Tambwe alicheza Simba kwa msimu mmoja na kufunga mabao 19 yaliyomwezesha kuwa Mfungaji Bora, lakini timu yake ikamaliza katika nafasi ya nne Ligi Kuu.

Miezi michache baadaye straika huyo akaamua kwenda Yanga ambako amefanikiwa kuweka rekodi ya aina yake huku akiipiga pini timu yake ya zamani ya Simba ambayo sasa imekwenda misimu mitano bila kutwaa taji la Ligi Kuu.

Kwanza, Tambwe alipotua tu Yanga katika msimu wake wa kwanza aliifungia mabao 13 yaliyoiwezesha kutwaa taji la Ligi Kuu ikiwa ni miezi sita tu tangu alipojiunga na timu hiyo.

Kama hiyo haitoshi, msimu uliopita Tambwe alifunga mabao 21 yaliyoipa Yanga taji jingine la Ligi Kuu na Jumanne iliyopita alifunga bao pekee la ushindi dhidi ya Toto Africans ambalo limeipa Yanga taji jingine la Ligi Kuu.

Hii inamfanya Tambwe kushinda mataji matatu katika kipindi cha miaka miwili na nusu tu aliyocheza Yanga hivyo kuwaacha katika mataa nyota aliocheza nao Simba.

Tambwe ambaye amefikisha mabao 11 sasa huku akibakiwa na mechi moja ya mwisho itakayochezwa kesho Jumamosi dhidi ya Mbao FC, alisema kuwa ni mtihani mkubwa kwake kujihakikishia kumaliza mbio za Mfungaji Bora kutokana na wachezaji waliomtangulia, hivyo ili aweze basi ni lazima apambane sana mechi ya mwisho jambo ambalo pia amesema ni rahisi.

“Nasikia furaha sana kuwa miongoni mwa wachezaji walioipa ubingwa Yanga kwa mara ya tatu mfululizo, hilo linanifariji hasa mimi kuipa ubingwa huo kwa kufunga bao muhimu, ligi ilikuwa na changamoto nyingi sana ambazo zilisababisha iwe ngumu. Unajua timu yetu tumepitia kwenye matatizo mengi ambayo yalitufanya tukomae zaidi katika kupambana na tumefanikiwa,” alisema.

“Mara nyingi huwa naweka nia na sio kwa mechi za kutwaa ubingwa pekee ila ni kila mechi ninayopata nafasi ya kucheza, napenda kufunga na ndiyo kazi na furaha yangu.  Mechi ya mwisho itakuwa ngumu sana kwetu watakuja wakiwa wamepania ingawa lengo letu ni kushinda,” alisema.