Juuko ametua mwanangu

KATUA mwanangu. Baada ya Simba kuaibishwa na beki yake ya kati katika mchezo wao dhidi ya Yanga juzi Jumamosi, beki wao kisiki, Juuko Murshid amerejea nchini na fasta akabidhiwa kwa kocha Joseph Omog.

Mcameroon huyo amepewa kati ya kuamua hatma yake klabuni hapo baada ya beki huyo kuchelewa kuripoti tangu ilipomalizika michuano ya Afcon 2017 nchini Gabon.

Kuumia kwa Method Mwanjali, Simba ilikosa beki wa kiwango cha juu wa kuidhibiti Yanga hivyo kuwatumia Novatus Lufunga aliyeshindwa kumudu mchezo huo na Janvier Bokungu aliyepewa kadi nyekundu.

Beki huyo raia wa Uganda alitakiwa kujiunga na Simba tangu timu yake ya taifa kutolewa hatua ya makundi ya Afcon, lakini aliingia mitini na kukata mawasiliano na mabosi wake, lakini ujio wake umeleta nafuu Msimbazi.

Ikumbukwe pia alipata msiba wa watoto wake watatu mapacha waliozaliwa mwishoni mwa mwaka jana.

Rais wa Simba, Evans Aveva alithibitisha kuwasili kwa Juuko na wamemkabidhi Omog kuamua hatma yake kama atacheza ama la.