JKT Ruvu sababu kibaaoo

Friday May 19 2017

 

By MWANAHIBA RICHARD

MAAFANDE wa JKT Ruvu wameshuka daraja baada ya kushiriki Ligi Kuu Bara kwa miaka 17, lakini wamesema kwamba kilichowashusha ni ufundi pekee kwa kutoka sare mechi 14 wakishinda tatu tu huku wakishinda mechi 12 hadi sasa.

JKT Ruvu imebakiza mchezo mmoja dhidi ya Ndanda FC mechi itakayochezwa ugenini ambapo itakuwa ni vigumu kwa maafande hao kuwafunga Ndanda wakiwa nyumbani.

Mbali na hilo, JKT Ruvu ipo katika hatari ya kuwapoteza nyota wake watatu ambao ni washambuliaji; Saady Kipanga, Atupele Green na kiungo Hassan Dilunga ambao si waajiriwa wa jeshi hilo na mikataba yao inamalizika sasa.

Afisa Mteule Daraja la Pili ambaye ndiye Msemaji wa timu hiyo, Costantine Masanja, alisema: “Hatukuwa na timu mbaya ila kilichotushusha kiukweli ni suluhu nyingi, wakati sisi tunatoka suluhu wenzetu walikuwa wanashinda, hivyo isingekuwa rahisi kwetu kupambana zaidi.

“Kuna wachezaji ambao mikataba yao inamalizika na si waajiriwa wa jeshi ila asilimia kubwa tuna hazina ya wachezaji ambao wameajiriwa maana sera yetu ya jeshi ni michezo.

“Hao ambao mikataba yao inamalizika tutazungumza nao ligi ikiisha kwa maana kwamba tukimaliza mechi ya mwisho maana kuna mwingine anaweza kukubali kubaki ama kuondoka.”