Ile sauti ni ya Steve Nyerere

Msanii  Steve Nyerere

Muktasari:

  • Katika mazungumzo hayo, msanii huyo anasikika akieleza jitihada alizofanya kuwashawishi wabunge na mawaziri kumsaidia Wema Sepetu aliposhikiliwa na jeshi la Polisi kutokana na tuhuma za kutumia dawa za kulevya.

MSANII Steve Nyerere ameibuka kutoa ufafanuzi wa mambo mbalimbali baada ya kusambaa kwa sauti anayosikika akizungumza na mama mzazi wa Wema Sepetu.

Katika mazungumzo hayo, msanii huyo anasikika akieleza jitihada alizofanya kuwashawishi wabunge na mawaziri kumsaidia Wema Sepetu aliposhikiliwa na jeshi la Polisi kutokana na tuhuma za kutumia dawa za kulevya.

“Naomba ukweli usipindishwe sauti ile ni yangu, maneno yale yalikuwa ya uongo niliyatoa kumtuliza mama na kujaribu kumzuia Wema asiondoke CCM maana walishaanza kusema akitoka ndani wanahamia Chadema,”alisema

“Namuomba radhi Rais Magufuli kwa kuwahusisha katika suala hili mawaziri wake aliowaamini na kuwateua kwenye nafasi nyeti nilifanya hivyo kwa kulinda heshima ya chama changu maana sikuwa na namna ya kufanya kama binadamu.”

Kuhusiana na madai ya kuwashawishi wabunge wajadili suala la Wema bungeni, Steve Nyerere alisema: “Namuomba radhi Spika kwa kusema niliwashinikiza wabunge kwa kuwa sina uwezo, ujanja wala mamlaka hayo, nilisema uongo.”

Aidha alikanusha kuwa amevunja uhusiano na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Paul Makonda; “Nje ya kazi yake Makonda ni ndugu yangu siwezi kugombana naye tunazungumza vizuri kabisa, niko naye bega kwa bega na ninaunga mkono jitihada zake za kupambana na dawa za kulevya.”

Wakati akiendelea na mazungumzo hayo, msanii huyo alishindwa kujizuia na kujikuta akidondosha machozi huku akimtupia lawama mama Wema kwa kitendo alichomfanyia.

“Hadi sasa najiuliza kwanini nirekodiwe? Mama ni muuaji hakuwa na nia njema na mimi, je ningeongea matusi mle ingekuwaje. Nimepata uchungu sana maana niliamini nilikuwa naongea na mama yangu ndiyo maana nikajiachia.

“Jina hili nimelitafuta kwa miaka 25, halafu leo mama anakuja kunichafua, napitia kipindi kigumu mno, lakini namwachia Mungu kwa kuwa nilifanya yote hayo kwa kumkumbatia Wema malipo yake ndio haya.”