Ibrahimovic ajutia kumjeruhi Mings

Monday March 6 2017

Mshambuliaji wa Manchester United, Zlatan

Mshambuliaji wa Manchester United, Zlatan Ibrahimovic 

London, England. Mshambuliaji wa Manchester United, Zlatan Ibrahimovic amesema yupo tayari kutekeleza adhabu iwapo itatolewa na Chama cha Soka England (FA) kutokana na kumchezea rafu mchezaji wa Bournmouth, Trone Mings.

Nyota huyo wa Manchester United, Ibrahimovic alisema atakubaliana na adhabu atakayopewa kutokana na kumpiga kiwiko mchezaji huyo.

Balaa hilo lilimkumba Mings wakati timu hizo zilipokutana  kwenye mchezo wa Ligi Kuu England na timu hizo zilitoka sare ya bao 1-1 mwishoni mwa wiki iliyopita.

Hata hivyo, Mings alilaumiwa kutokana na kumkanyaga kichwa Ibrahimovic kabla naye hajampiga na kiwiko, lakini inaelezwa kwamba kila mtu hakukusudia kuchezea vibaya mwenzake.

Pia, chama cha soka nchini humo kinatarajiwa kuchukua hatua zaidi za kinidhamu dhidi ya Ibrahimovic.

“Ninaheshimu kila uamuzi” alisema mchezaji huyo mwenye miaka 35.

Aliongeza, “ Sipo hapa kwa ajili ya kumlaumu yeyote. Haikuwa lengo langu kufanya vile.”

Ibrahimovic iliikosesha penalti Manchester United, huku kikosi cha Jose Mourinho mara nyingine kikibakia kwenye nafasi ya sita.

Hadi sasa Manchester United ina tofauti ya pointi 14 dhidi ya kinara Chelsea, huku ikiwa nyuma kwa pointi tatu kwa Livepool.

Habari za kufungiwa Ibrahimovic zimesambaa kwenye mitandao ya kijamii na vyombo vya habari. Mchezaji huyo mpaka sasa ameshafunga mabao 26 katika michezo 39 aliyocheza kwenye mashindano yote kwa msimu mmoja tangu alipotua Uwanja wa Old Trafford.