He! Simba kaja kweli

Muktasari:

  • Kumbe Simba walisikia kejeli hizo na jana jioni Uwanja wa Amaan mjini hapa ikafanya kweli ikainyuka Jang’ombe Boys 2-0 na kumaliza kinara Kundi A, kitu kilichowafanya mashabiki Yanga kushtuka.
  • Unajua kwanini? Kwa namna Yanga ilivyocheza na Azam na kukoga bao nyingi zimewafanya mashabiki hao kujiuliza ; “Eeh! Simba kumbe kaja kweli’, lakini wakajipa moyo kwamba liwalo na liwe, lazima kesho Jumanne jioni kieleweke.

YANGA juzi usiku walifumuliwa mabao 4-0 na Azam, mashabiki wao Dar es Salaam wakajitetea kuwa wametaka washike nafasi ya pili ili wapate fursa ya kumalizana mapema na Simba.

Kumbe Simba walisikia kejeli hizo na jana jioni Uwanja wa Amaan mjini hapa ikafanya kweli ikainyuka Jang’ombe Boys 2-0 na kumaliza kinara Kundi A, kitu kilichowafanya mashabiki Yanga kushtuka.

Unajua kwanini? Kwa namna Yanga ilivyocheza na Azam na kukoga bao nyingi zimewafanya mashabiki hao kujiuliza ; “Eeh! Simba kumbe kaja kweli’, lakini wakajipa moyo kwamba liwalo na liwe, lazima kesho Jumanne jioni kieleweke.

Mchezo wa jana ulianza kwa kasi, dakika 10 za mwanzo Simba ilifanya mashambulizi mara mbili kupitia kwa Mzamiru Yassin lakini safu ya ulinzi ya Boys ilikuwa imara kutuliza presha hiyo. Boys ilitulia na kufika pia langoni mwa Simba mara moja lakini shuti la Juma Ali lilipaa juu ya lango.

Mavugo aliwainua mashabiki wa Simba dakika ya 11 akimalizia mpira uliookolewa na kipa wa Boys, Hasham Haroub kufuatia shuti kali la Shiza Kichuya.

Baada ya bao hilo, Boys walitulia na kutaka kusawazisha lakini juhudi za Khamis Makame ‘Rais’ dakika za 24 na 32 hazikuwa na madhara makubwa kwa Simba.

Kipindi cha pili Simba iliyoonekana kupania kukutana na Yanga nusu fainali ilimtoa Mzamiru na kumuingiz kiungo Mghana, James Kotey mabadiliko yaliyozaa matunda kwa Mavugo kufunga bao la pili dakika ya 54 kwa juhudi binafsi baada ya kuipasua ngome ya Boys na kupiga shuti kali. Simba pia iliwapumzisha Mavugo, Juma Liuzio na Kichuya na kuingia Jamal Mnyate, chipukizi Mosses Kitandu na Haji Ugando. Boys iliwapumzisha Juma Ali na Mkubwa Aboubakar wakaingia Yacoub Amour na Juma Suleiman. Simba ilimtoa Janvier Bokungu akaingia Vincent Costa. Boys ilimtoa Ali Badru akaingia Hamidu Ramadhan.

KAULI YA MASHABIKI

Hassan Ameir, mdau wa soka visiwani hapa alisema anaitazama Simba kama timu inayocheza kwa umoja zaidi hivyo ina nafasi kubwa ya kuwafunga Yanga kesho.

“Yanga bado hawajaweza kucheza kitimu tofauti na Simba inayoonekana imekamilika, inacheza kwa ushirikiano,” alisema Ameir wakati Issa Ali Issa alisema mara nyingi mechi ya Simba na Yanga haitabiriki hivyo ni vigumu kusema nani anaweza kupoteza hata kama Yanga ilipoteza kwa Azam.

SIMBA NA YANGA

Hii ni mara ya nne Simba na Yanga kukutana visiwani hapa, mara ya kwanza mwaka 1975 katika fanali ya Kombe la Kagame na Yanga kushinda mabao 2-0 yaliyofungwa na Gibson Sembuli na Sunday Manara.

Zilikutana tena fainali nyingine ya Kagame mwaka 1992, dakika 120 ziliisha kwa sare ya 1-1 na kwenye penalti Simba ilishinda 5-4, kabla ya kukutana tena fainali za Kombe la Mapinduzi 2011. Simba ilishinda 2-0.

Wakati Simb na Yanga zikitarajiwa kukutana kesho saa 10 jioni usiku itakuwa zamu ya Azam vinara wa Kundi B dhidi ya mshindi wa mechi ya usiku wa jana kayi ya URA ya Uganda na Taifa Jang’ombe.