Hazard anakwenda Madrid kimyakimya

MADRID, HISPANIA. HILI dili linafanyika kwa siri na kilichofichuka ni kwamba Real Madrid wapo katika hatua za mwisho mwisho kabisa za kukubaliana na staa wa Chelsea, Eden Hazard.

Kuna taarifa zimetoka Hispania limedai kwamba kuna kishindo kikubwa kitatokea kwenye dirisha la uhamisho lijalo baada ya maofisa wa klabu hizo mbili, Chelsea na Real Madrid kuwa na vikao vyao vya siri kuhusu Hazard.

Hazard kwa muda mrefu sana amekuwa akihusishwa na Real Madrid, lakini sasa dili hilo la kutua Santiago Bernabeu linaonekana limekuwa siriazi.

Kiwango chake cha msimu huu kwenye Ligi Kuu England huku akiwa amefunga mabao 10 katika michuano yote aliyocheza kimemshawishi kocha Real Madrid, Zinedine Zidane na kuamini sasa kimefika kipindi mwafaka cha kuinasa huduma ya Mbelgiji huyo. Hazard hana siri kwamba anamkubali sana Zidane na jambo hilo linaweza kumsukuma akaenda kuungana naye huko Bernabeu.

Uhamisho huo utamfanya Hazard kwenda kucheza na wachezaji bora kabisa duniani, Cristiano Ronaldo na Gareth Bale na kwamba wataifanya safu ya ushambuliaji ya Los Blancos kuwa na makali ya wembe. Karim Benzema maisha yake yanaonekana kufika mwisho Bernabeu, huku Ronaldo kasi yake imepungua, hivyo wababe hao wa Hispania wanaamini Hazard atakuwa silaha yao mpya.