Ghafla Majimaji wamekuwa matajiri Dar, Simba wajilipua

Muktasari:

  • Omog ameiambia Mwanaspoti kwamba Ajib kama ilivyokuwa kwa Fredrick Blagnon ambao wote wana kadi mbili za njano wapo katika mpango wake wa kucheza mchezo wa leo, ambao endapo watapewa kadi yoyote wanaweza kukosa mechi ya Yanga Oktoba mosi.

INAWEZEKANA leo kwenye Uwanja wa Uhuru ukakumbana na maajabu ambayo ulikuwa hutazamii. Kuna mambo mawili, Majimaji ambayo haijawahi kuambulia hata sare tangu msimu uanze wanaweza kushangaza umma kwa kufufukia mikononi mwa Simba.

Majimaji iliyokuwa inagongea mpaka msosi, iliyokuwa haina nauli imekumbana na zali jijini Dar kwa kunasa mdhamini mpya na kuwa matajiri ghafla. Achana na sapoti ya chinichini wanayopewa na mashabiki wa Yanga, mdhamini mpya amewarudishia kocha wao wa zamani, Kally Ongalla ambaye leo atakuwa kwenye benchi rasmi.

Lakini usifikiri Mnyama amelala. Simba wamepania kushusha kipigo cha ajabu kwa vibonde hao ili kuishtua Yanga wanayokutana nayo wikiendi ijayo kwenye mechi ya watani wa jadi.

Iko hivi. Kampuni ya GSM imeweka nguvu kwenye mechi hii na inataka kukata ngebe za Simba ambao wamepania kutwaa ubingwa msimu huu, we fikiria Majimaji iliyokuwa inapiga matizi kwenye viwanja vya vumbi sasa imefanyia mazoezi pale kwenye kapeti ya Ghymkana ambapo gharama yake kwa siku moja ni Sh 250,000.

Ujio wa GSM umewatisha Simba ambapo wameanza kupanga mbinu mbalimbali na kuongeza nguvu kwenye mipango yao ya ushindi. Mwenyekiti wa klabu hiyo, Humphrey Milanzi aliliambia Mwanaspoti kuwa; “Tutasaini mkataba na GSM baada ya mechi ya kesho (leo) na Simba, ila tunaweza kusema kila kitu kipo vizuri na ni kama vile wameanza kufanya kazi, wao ndiyo wamelipia uwanja wa mazoezi pale Gymkhana pamoja na kumrudisha kocha Kally. Kiukweli morali ya wachezaji wetu ipo juu maana hata kwenye masilahi yao hasa mshahara watapata kwa wakati.

“Tumepata matokeo mabaya mechi zote ila mashabiki wa soka wasishangae sisi kupata ushindi dhidi ya Simba kwani, yote yanawezekana. Mwanzo wachezaji morali yao ilishuka mno, hatukuwa na uwezo wowote wa kuwawezesha tofauti na sasa ambapo kuna baadhi ya mambo yamekaa sawa kupitia udhamini huo,” alisema Milanzi

OMOG AJILIPUA KWA OMOG

Mashabiki wa Simba wanatamani hata kumpigia magoti, Kocha wao Joseph Omog ili asimchezeshe mshambuliaji Ibrahim Ajib katika mchezo wa leo dhidi ya Majimaji kwa hofu ya kumkosa dhidi ya Yanga. Simba wana wasiwasi kwamba asije akaonyeshwa kadi akaikosa Yanga.

Omog ameiambia Mwanaspoti kwamba Ajib kama ilivyokuwa kwa Fredrick Blagnon ambao wote wana kadi mbili za njano wapo katika mpango wake wa kucheza mchezo wa leo, ambao endapo watapewa kadi yoyote wanaweza kukosa mechi ya Yanga Oktoba mosi.

“Siwezi kuhofia kumkosa mchezaji dhidi ya Yanga, nafahamu kwamba hao wawili wana kadi mbili za njano lakini uamuzi wa kucheza upo wazi watacheza,” alisema Omog ambaye anaijua vizuri soka ya Tanzania na siasa za nje ya uwanja za Simba na Yanga.

“Tuna kikosi kipana kama watapita katika majina ninaowataka kucheza watacheza na kama wakipewa kadi nitatafuta watu wengi wa kucheza nafasi zao na bado tunaweza kushinda lakini kama watacheza wanatakiwa kuwa makini.”

“Mchezo muhimu kwetu sasa ni dhidi ya Majimaji, hawa Yanga waacheni kwanza nafikiri nitawaongelea kwa undani Jumamosi jioni, lakini kwa sasa ninachoweza kusema nawajua na ninataarifa zao za kutosha.”