Fifa: Hatujaona rufaa ya Simba

Muktasari:

Msemaji wa Fifa, Segolene Valentin aliliambia Mwanaspoti jana saa 9.15 Alasiri kwamba hadi muda huo hakukuwa na barua yoyote ya Simba iliyokuwa imewasili.

SHIRIKISHO la Soka Duniani (Fifa) limesema mpaka jana Alasiri halikuwa limepokea malalamiko yoyote kutoka klabu ya Simba licha ya kwamba viongozi hao wamezidi kusisitiza mzigo tayari umetua Zurich yalipo makao makuu ya shirikisho hilo.

Msemaji wa Fifa, Segolene Valentin aliliambia Mwanaspoti jana saa 9.15 Alasiri kwamba hadi muda huo hakukuwa na barua yoyote ya Simba iliyokuwa imewasili.

Hata hivyo, taarifa kutoka kampuni ya kusafirisha mizigo na barua ya DHL ilionyesha kwamba mzigo wa vielelezo vya ushahidi wa kesi ya Simba dhidi ya Kagera Sugar ulikuwa umetua mjini Zurich saa tatu asubuhi. Vielelezo hivyo vyenye uzito wa Kilogramu 1.5 vilitumwa Alhamisi Mei 18 jijini Dar es Salaam kwa Kampuni hiyo huku barua ya Simba iliyosaniwa na Katibu Mkuu, Hamisi Kisiwa ikitangulia Fifa siku hiyo. Kwa mujibu wa taarifa ya usafirishaji kutoka DHL, mzigo huo ulipita mjini Amsterdam, Uholanzi siku ya Ijumaa Mei 19 kabla ya kusafirishwa kenda Brussels Ubelgiji na kisha Leipzig Ujerumani siku ya Jumapili. Mzigo huo ulitua katika Mji wa Basel nchini Uswizi jana Jumatatu saa 12.42 asubuhi kabla ya kusafirishwa kwenda mjini Zurich na ulitua saa 2.26 asubuhi na kuchukuliwa na kufikishwa makao makuu ya Fifa saa 3.45 asubuhi.