Dr Dre matatani, atiwa pingu

Dr Dre

Muktasari:

 RAPA na mtayarishaji muziki maarufu, Dr Dre ameingia katika mzozo na polisi baada ya ugomvi ulioibuka nje ya  mjengo wake wa kifahari, jana

Jumatatu.

NEW YORK, MAREKANI. RAPA na mtayarishaji muziki maarufu, Dr Dre ameingia katika mzozo na polisi baada ya ugomvi ulioibuka nje ya  mjengo wake wa kifahari, jana

Jumatatu.

Dr Dre 51, rapa mwenye watoto watano aliozaa na wanawake tofauti, alikamatwa na kuonekana nje ya nyumba yake akiwa amefungwa pingu.

Ilidaiwa kwamba Dr Dre aligombana na mtu ambaye alizuia njia kwa kupaki gari vibaya na hiyo kuwa sababu ya ugomvi na rapa huyo ambaye mwaka 2014 alishika nafasi ya kwanza kwa utajiri miongoni mwa marapa duniani.

Inadaiwa Dr Dre alimfokea mtu huyo akimtaka aondoke lakini mtu huyo akawa mbishi na ndipo Dr Dre alipomfuata na kumsukuma, tukio ambalo mtu huyo alilirekodi kwa simu.

Baadaye mtu huyo alipiga simu polisi akilalamika kutishiwa kwa silaha ya moto: "Ni tukio jingine tena la mtu mweusi na silaha."

Hata hivyo polisi walipofika hawakuona silaha huku Dr Dre mwenyewe akikana kumtishia mtu yeyote na silaha. Baadaye rapa huyo aliachiwa ingawa huenda akashitakiwa iwapo ushahidi wa awali utaona kama ana kosa la kujibu.