Dili la Majimaji mikononi mwa Simba

Muktasari:

Wanalizombe ndio wanaoburuza mkia kwa sasa katika Ligi Kuu Bara ikiwa haijashinda mechi hata moja, lakini kama dili lao la GSM litatiki wataogelea neema na kuachana na kilio cha ukata kisichoisha tangu msimu huu uanze.

MAJIMAJI imekuwa ikilia njaa, lakini hivi karibuni iliangukiwa na zali baada ya kampuni ya GSM kutaka kuidhamini ila dili hilo litakamilika mara baada ya mechi ya Jumamosi dhidi ya Simba.

Wanalizombe ndio wanaoburuza mkia kwa sasa katika Ligi Kuu Bara ikiwa haijashinda mechi hata moja, lakini kama dili lao la GSM litatiki wataogelea neema na kuachana na kilio cha ukata kisichoisha tangu msimu huu uanze.

Mwenyekiti wa timu hiyo, Humphrey Milanzi, alisema wamekubaliana na mdhamini huyo mtarajiwa kuwa watamalizana baada ya mchezo huo utakaopigwa jijini Dar es Salaam.

“Mambo ya kuingia mkataba na GSM ni baada ya mechi hiyo kwa sasa hatuwezi kudili na mambo mawili kwa wakati mmoja. Najua mechi ni ngumu ila vijana wana morali ya kupambana,” alisema.

Alisema timu imeondoka jana Songea kujana Dar es Salaam na kwamba, licha ya Simba kuwa vizuri kwa sasa, wenyewe wataangalia kupambana zaidi ili kupata ushindi.

“Kwa sasa si kazi rahisi kuifunga Simba, ila wachezaji tumewajenga saikolojia kuingia vitani na kamwe hawataangalia matukio ya nyuma bali kuingia uwanjani kupambana kushinda mchezo huu,” alisema