Dante ashtukia soka la Kocha Lwandamina

Beki wa Yanga, Andrew Vincent ‘Dante’

Muktasari:

Dante aliongeza kuwa kocha huyo anapenda timu icheze mpira wa chini kwa pasi fupi fupi na siyo kuwa na papara na ndiyo maana hata mazoezi yake ni ya kuchezea mpira sana kuliko kitu kingine.

BEKI wa Yanga, Andrew Vincent ‘Dante’ ameshtukia jambo kwa kocha wake George Lwandamina na kudai kuwa kocha huyo amekuwa akiwasoma sana wachezaji wake kila anapotoa mazoezi yake jambo ambalo linaonyesha ukizubaa unaweza ukakaa benchi.

Dante aliongeza kuwa kocha huyo anapenda timu icheze mpira wa chini kwa pasi fupi fupi na siyo kuwa na papara na ndiyo maana hata mazoezi yake ni ya kuchezea mpira sana kuliko kitu kingine.

“Kocha anaonekana kuwa makini sana kwa wachzaji kwani huwa anatoa mazoezi madogo madogo lakini najua anafanya hivi ili kutusoma wachezaji jinsi tulivyo kwasababu hajatuzoea hivyo anafanya hivi atuweke karibu na kutusoma na ukijisahau benchi linakuhusu,”alisema Dante.

“Anapenda sana tucheze mpira hasa wa chini, hapendi mpira wa juu juu na ndiyo maana katika mazoezi yake utakuta mara nyingi tunachezea mpira na kisha mechi ya sisi kwa sisi kutuangalia zaidi,”alisema.

Lwandamina amekuwa na mazoezi na Yanga kwa wiki moja sasa akijaribu kuwasoma nyota hao ili kuona ni nani anaweza kuwa msaada mkubwa katika mzunguko wa pili ambao utaanza wiki moja ijayo huku Yanga ikiwa nyuma kwa pointi mbili dhidi ya vinara wa ligi hiyo Simba.

Kocha huyo kutoka Zambia anaaminika kuwa muumini wa nidhamu na muda.