Chirwa sasa anateleza tu

Straika wa Yanga, Obrey Chirwa.

Muktasari:

Mzambia huyo aliifungia Yanga bao moja katika mchezo huo uliochezwa kwenye Uwanja wa CCM Kirumba, jijini hapa likiwa ni bao lake la pili tangu asajiliwe na Yanga akitokea FC Platinum ya Zimbabwe.

STRAIKA aliyekuwa akipondwa kwa kushindwa kufunga mabao Yanga, Obrey Chirwa kwa sasa anateleza tu, jana Jumatano ametupia tena bao wakati timu yake ikipata ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Toto Africans katika mechi ya Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) Bara.

Mzambia huyo aliifungia Yanga bao moja katika mchezo huo uliochezwa kwenye Uwanja wa CCM Kirumba, jijini hapa likiwa ni bao lake la pili tangu asajiliwe na Yanga akitokea FC Platinum ya Zimbabwe.

Chirwa alifunga bao hilo katika dakika ya 28 akiunganisha kwa kichwa mpira wa krosi ya Donald Ngoma na kuzaa bao lililodumu hadi wakati wa mapumziko.

Winga Simon Msuva aliiongezea Yanga bao dakika ya 56 baada ya Deus Kaseke kuchezewa madhambi na Yusuf Mlipili, hilo likiwa bao la 51 kwa mchezaji huyo tangu ajiunge na Yanga mwaka 2012 akitokea Moro United.

Licha ya ushindi huo, Yanga inapaswa kujilaumu kwa kushindwa kupata idadi kubwa ya mabao kwenye mchezo huo ambao ulipooza dakika za awali kabla ya kuchanganya kadri muda ulivyokuwa ukisonga.

Kwa ushindi huo Yanga imefikisha pointi 18 na kurejea nafasi ya tatu ikiitoa Kagera Sugar ambayo juzi Jumanne ilikwea nafasi hiyo baada ya kuifunga JKT Ruvu bao 1-0 kwenye Uwanja wa Mabatini, Pwani.

Yanga: Deo Munishi, Hassan Kessy, Oscar Joshua, Andrew Vincent, Kelvin Yondani, Mbuyu Twite, Simon Msuva/ Simon Matheo, Haruna Niyonzima, Donald Ngoma /Thabani Kamusoko, Obrey Chirwa na Deus Kaseke/Juma Mahadhi.

Toto: David Kissu, Salum Chuku, Yusuf Mgeta, Carlos Protas, Yusuf Mlipili, Ramadhani Malima/Hamim Abdul, Soud Mtegeta/ Frank Sekule Reliant Lusajo, Waziri Junior, William Joshua na Jaffar Mohammed/Mohammed Athuman

Katika mechi nyingine za VPL, Chama la Wana, Stand United jana ilionja machungu ya ligi hiyo kwa mara ya kwanza baada ya kufungwa mabao 2-1 na Prisons kwenye Uwanja wa Sokoine, Mbeya kama anavyoripoti Godfrey Kahango.

Prisons ilipata mabao yake kupitia kwa Salum Bosco na Lambart Sabianka wakati Stand ilipata bao la kufutia machozi kwa mkwaju wa penalti iliyofungwa na nahodha wake, Jacob Massawe.

Matokeo mengine ya mechi za jana Majimaji chini ya Kally Ongalla ilitoka mkiani baada ya kupata ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Africans Lyon mjini Songea, huku Ndanda na Mbeya City zikitoka sare ya bao 1-1 kama ilivyokuwa kwa pambano la Ruvu Shooting na Mwadui Shinyanga.