Chirwa mbona ndo kwanza anaanza

Muktasari:

Pluijm ndiye aliyempendekeza Chirwa asajiliwe na Yanga mwezi Juni mwaka jana lakini akakutana na maisha magumu baada ya kucheza mechi 12 za mwanzo bila kufunga bao hata la kuotea.

MKURUGENZI wa Ufundi wa Yanga, Hans Van Pluijm amefichua siri kuwa uvumilivu wa klabu hiyo kwa straika Obrey Chirwa umezaa matunda kwani sasa ndiyo ameanza kuthibitisha kuwa yeye ni bonge la straika na haikuwa bahati mbaya akasajiliwa klabuni hapo.

Pluijm ndiye aliyempendekeza Chirwa asajiliwe na Yanga mwezi Juni mwaka jana lakini akakutana na maisha magumu baada ya kucheza mechi 12 za mwanzo bila kufunga bao hata la kuotea.

Hata hivyo baadaye Chirwa alifanikiwa kufunga mabao matano katika mechi za ligi kuu kwenye mzunguko wa kwanza kabla ya kupoteza tena makali yake jambo ambalo liliwashawishi viongozi wa Yanga kutaka kumtoa kwa mkopo katika usajili wa dirisha dogo.

Hata hivyo Chirwa amefanikiwa kufufua makali yake baada ya kufunga mabao manne katika mechi tatu za mwisho jambo ambalo limemgusa Pluijm ambaye amedai kuwa bado straika huyo ana vitu vingi vya kuifanyia Yanga.

“Bado ana vitu vingi. Kama nilivyosema awali kuwa ni straika makini, anajua kufunga na ana uwezo mkubwa wa kutengeneza nafasi pia,” alisema Pluijm ambaye alishinda mataji matano na Yanga.

“Alikuwa anahitaji muda kuzoea timu, kuwazoea wachezaji wenzake na pia kulizoea soka la Tanzania, Kwa sasa yupo katika ubora ambao niliuona mwanzo wakati napendekeza asajiliwe,” alisema Pluijm.