Chezea Manji wewe!

MILIONI 10 Kiwango cha dhamana alichowekewa Manji ili kuachiwa huru mtaani. Fedha hizo zililipwa na Katibu Mkuu wa Yanga, Boniface Mkwasa.

Muktasari:

  • Manji, kiongozi mstaafu wa kampuni tanzu ya Quality Group inayoidhamini Yanga, amefanikiwa kurudi uraiani baada ya kushikiliwa kwa siku saba akituhumiwa kujihusisha na matumizi ya dawa za kulevya.

MWENYEKITI wa Yanga, Yusuf Manji jana Alhamisi mchana aliachiwa kwa dhamana kwenye Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu lakini tangu asubuhi hadi jioni kulikuwa na vituko vya aina yake.

Moja ya vituko vilivyokuwa mahakamani hapo ni mashabiki wa Yanga waliojisahaulisha msoto aliopata tangu aliposhikiliwa Alhamisi iliyopita, wakaanza kuwakejeli wenzao Simba kwamba: “Msiyempenda katoka mtakiona cha moto Taifa,” na wengine “Chezea Manji, kaingia na Ranger Rover katoka na Hammer.”

Manji, kiongozi mstaafu wa kampuni tanzu ya Quality Group inayoidhamini Yanga, amefanikiwa kurudi uraiani baada ya kushikiliwa kwa siku saba akituhumiwa kujihusisha na matumizi ya dawa za kulevya.

Bilionea huyo aliugua ghafla wikiendi iliyopita akiwa ameshikiliwa Kituo Kikuu cha Polisi Dar es Salaam na kukimbizwa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili kitengo cha Moyo cha Jakaya Kikwete na juzi Jumatano jioni aliruhusiwa lakini akarudishwa Polisi kabla ya kuzidiwa tena usiku wa kuamkia jana na kurudishwa hospitalini. Kamanda wa Polisi wa Kanda Maalum, Simon Sirro alitangaza juzi jioni kwamba jana Manji angefikishwa mahakamani kusomewa mashtaka yake.

Awali ilisemekana kwamba jana huenda angesomewa mashtaka akiwa hospitali kabla ya utaratibu kubadilishwa na kuchukuliwa na gari kutoka hospitali akisindikizwa na polisi kupelekwa Mahakama ya Kisutu kusomewa mashtaka. Aliwasili hapo saa 7:55 mchana na kukumbana na umati wa mashabiki na viongozi karibu wote wa juu wa Yanga na wakuu wa kamati mbalimbali za klabu hiyo.

Wakati Manji akifika mahakamani, ulinzi mkali wa polisi walio na silaha waliongoza msafara huku gari yake binafsi iliyombeba ikiwa kati, nyuma gari nyingine ndogo ya serikali.

Akisomewa mashtaka hayo na karani wa mahakama, Sarah Mlokozi mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi, Cyprian Mkeha, alisema shtaka linalomkabili Manji ni kutumia madawa ya kulevya aina ya Heroin madai ambayo Manji aliyakana.

Baada ya kusomwa shtaka hilo wakili wa serikali Osward Tibabyekyoma akisaidiwa na Shadrack Kimaro  walimfungulia hati ya dhamana mshtakiwa kwa kigezo kuwa upelelezi wa kosa hilo bado unaendelea.

Awali wakili aliyekuwa akimtetea Manji, Alex Mgongolwa alimuomba hakimu kumfungulia mteja wake hati ya dhamana kwa kuwa ni mtumishi wa watu hususani kuwa diwani Kata ya Mbagala ombi ambalo Hakimu Mkeha alilikubali.

Baada ya hakimu kukubali ombi hilo, Manji alitakiwa kudhaminiwa na mtu mmoja na Katibu Mkuu wa Yanga Charles Mkwasa alichukua jukumu hilo huku Manji mwenyewe akibeba jukumu la kujidhamini kwa fedha Sh 10 milioni wakati shtaka hilo likipangiwa kutajwa tena Machi 16, 2017.

Wanachama wafurika
Mara baada ya Manji kuachiwa wanachama wa Yanga waliokuja mahakamani hapo walianza kuomba duwa kila mtu na dini yake wakishukuru mwenyekiti wao kuachiwa na baada ya Manji kuondoka mahakamani hapo akiwa katika gari yake ya kisasa aina ya Hammer T670 BBX wanachama hao walianza kuimba nyimbo za furaha.Bila kujali kwamba kiongozi huyo alisota mahakamani, kejeli nyingi zilitawala hasa kutokana na mashabiki wa Simba ambao walikuwa wakiwakejeli kwamba Manji angesota na wangewafunga.

Lakini Yanga walikuwa wakishangilia kwa kejeli huku viongozi waliojazana mahakamani hapo wakikumbatiana kupongezana kwani tangu asubuhi walionekana wakifanya vikao visivyoisha nje ya Hospitali ya Muhimbili na mahakamani hapo.

Waliokuwepo ni wajumbe la Baraza la Wadhamini, Mama Fatma Karume, Mzee Jabir Katundu, Makamu Mwenyekiti Yanga, Clement Sanga na wajumbe wa Kamati ya Utendaji, Hussein Nyika, Samuel Lukumay, Salum Mkemi na viongozi wengine wa matawi na wawakilishi wa wanachama.

HEROIN NI NINI?

Heroin ni aina ya dawa za kulevya ambazo watumiaji  hutumia kwa kuchoma sindano, kunusa au kuvuta, mtumiaji akifanya hivyo hujikuta katika hali ya kusinzia. Dawa hizo huingia haraka katika ubongo na kusababisha hali ya kusinzia inayomfanya mtu kuonekana kama yupo macho ama ananing’iniza kichwa kwa kusinzia. Matumizi makubwa ya dawa hizi humfanya mtu kupoteza fahamu

Kutokana na kemikali zilizopo katika dawa hizo, mtumiaji mara nyingi hukumbwa na muwasho wa ngozi hali inayomsababisha kujikuna mara kwa mara. Hadi mwaka 2015 watu zaidi ya milioni 17 duniani walikuwa wakitumia dawa hizo. Kwa mara ya kwanza zilitengenezwa nchini Ujerumani.

Awali dawa hizo zilitengenezwa kama mbadala wa dawa za kutuliza maumivu lakini baadhi ya watu waliozitumia walionekana kulala usingizi ambao siyo sawa na ule wa usiku.

Mara nyingi wanaosafirisha dawa hizi humeza kete hizo na kuzivusha kutoka nchi moja hadi nyingine na wakifika katika kituo humeza dawa za kuwafanya wazitoe kwa njia ya haja kubwa. Ni miongoni mwa dawa ghali zaidi ingawa pia kuna za bei rahisi ambazo inaelezwa zina madhara makubwa kwa watumiaji.