Cannavaro achimba mkwara Msimbazi

NAHODHA na beki wa kati wa Yanga, Nadir Haroub ‘Cannavaro’ amechimba mkwara mzito Msimbazi, akidai kuwa mechi baina yao ndio itakayoamua bingwa na wana hakika watawapiga tu, lakini ngoja waende wakafanye yao kwanza visiwani Comoro.

Yanga inaoongoza msimamo wa Ligi Kuu kwa sasa kwa tofauti na pointi moja mbele ya Simba, inatarajiwa kwenda Comoro wiki hii kucheza mechi yao ya kwanza ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya wenyeji wao, Ngaya De Mbe.

Cannavaro aliyetangaza atastaafu rasmi kucheza soka miaka mitatu ijayo,  alisema kutokana na ushindani uliopo kwenye ligi, mechi ya watani ndio itaamua ubingwa wa msimu huu, huku akitamba lazima washinde.

Mechi hiyo itapigwa Februari 25 wakati Yanga ikiwa imeshajua hatma yao ya ushiriki wa Ligi ya Mabingwa Afrika kwani, itakuwa imecheza mechi zote mbili dhidi ya Wacomoro.

“Sina wasiwasi kwa sababu najua wale ni wetu tutawapiga tu. Kwa kawaida mechi hiyo huwa na ushindani lakini  kwa uzoefu wangu nauchukulia wa kawaida tu, kikubwa ni kujiandaa na kila kitu kitakaa vizuri,” alisema Cannavaro.

Akizungumzia kiwango chake baada ya kukaa nje ya uwanja kwa kipindi kirefu, Cannavaro amesema ni hali ya kawaida ili kuwapa nafasi wengine lakini si kwamba kiwango chake kimeshuka.