Cannavaro: Simba mtaongoza ligi wakati tukisafiri tu

Monday February 13 2017

 

By KHATIMU NAHEKA, COMORO

BEKI na nahodha wa Yanga, Nadir Haroub ‘Cannavaro’ ameisikia dozi ya Simba ikiwachapa Prisons ya Mbeya mabao 3-0, kisha akatamka kwamba matokeo hayo hayajamshtua ila kuhusu Simba kuongoza ligi akajibu kuwa hilo litaendelea kutokea pale tu Yanga itakapokuwa katika majukumu ya Kimataifa.

Alisema mara baada ya timu yao kurudi nyumbani na kucheza mechi yao hawana wasiwasi kwamba watashinda na kuwarudisha watani wao katika nafasi yao waliyoizoea.

Beki huyo mkongwe alisema kwa sasa kikosi chao chini ya Kocha George Lwandamina kimeimarika na kwamba ni vigumu kuona matokeo mabaya katika mechi zao.

“Simba najua wataongoza ligi lakini nikwambie tu hawawezi kuongoza ligi kwasasa kama na sisi tutakuwa tunaendelea na ligi, wataendelea kusubiri tusafiri ili wao waongoze,” alisema Cannavaro.

“Tutachukua ubingwa msimu huu, tuna kocha mzuri ambaye katika kipindi kifupi ameweza kuijulia timu hatuoni kama kuna mchezo tutapoteza kirahisi, tunajua sasa tutakuwa na kiporo cha mchezo mmoja wanaweza kudhani tutapoteza, imani yangu ni kwamba tutashinda tu.