Busungu wa Yanga apelekwa kliniki

Muktasari:

Taarifa zilizopatikana wakati tukielekea mitamboni, zinasema Yanga ikiwa na nyota wake wote watatua bungeni Dodoma kabla ya kucheza mechi moja ya kirafiki na Polisi kati ya kesho na keshokutwa.

WAKATI straika wa Yanga, Malimi Busungu akipelekwa kwa mtaalamu wa saikolojia, kikosi kizima cha mabingwa hao wa Tanzania leo kinaanza safari ya kulipeleka kombe lao Bungeni Dodoma kabla ya kutua jijini Arusha.

Taarifa zilizopatikana wakati tukielekea mitamboni, zinasema Yanga ikiwa na nyota wake wote watatua bungeni Dodoma kabla ya kucheza mechi moja ya kirafiki na Polisi kati ya kesho na keshokutwa.

Taarifa hizo zinaongeza, baada ya mechi hiyo, itakwenda Arusha kucheza mechi nyingine wikiendi hii sambamba na kulitambulisha kombe lao jijini humo mbele ya mashabiki wao.

Hata hivyo, wakati kikosi hicho kikiondoka leo, straika wao, Busungu ambaye hivi karibuni picha zake zilisambaa mitandaoni zikimwonyesha akiwa kalewa, amepelekwa kliniki maalumu ya saikolojia ili kumsaidia kwa matatizo aliyonayo..

Meneja wa Busungu , Yahya Tastao ameliambia Mwanaspoti kuwa; “Nimemtafutia mtaalamu wa saiokolojia ili kumsaidia kumweka sawa kutokana na mambo yanayomvuruga kichwani kiasi cha kufanya vitu visivyo sahihi mbele za watu, ameanza kliniki hiyo wiki iliyopita na atakuwa akihudhuria mara mbili kwa wiki.

Busungu aliyeichezea Yanga msimu huu kwa dakika 35 tu, amedaiwa kuvurukwa kutokana na kitendo cha kukalia benchi, lakini meneja wake anaamini matibabu aliyomwanzishia yatamsaidia straika huyo aliyewahi kutamba na Mgambo JKT kurejea katika ubora wake wa zamani uliomfanya kuwa mmoja wa mastraika hatari katika Ligi Kuu Bara