Busungu kumbe aliwekwa ndani

MSHAMBULIAJI Malimi Busungu aliwekwa ndani baada ya kupata ajali na gari lake mkoani Morogoro alipokuwa njiani kuelekea Dodoma.

Akizungumza na Mwanaspoti alisema, baada ya kupata ajali alichukuliwa na kuwekwa ndani na polisi na kisha kutolewa kesho yake kutokana na mwendo kasi uliosababisha ajali.

Kuhusu kujiunga katika mazoezi na wenzake (Yanga) ambao wanaanza mazoezi leo Jumatatu alisema atajiunga baada ya kwenda kuripoti polisi kama alivyotakiwa.

“Bado nipo Morogoro, lakini nashukuru Mungu naendelea vizuri hivi sasa sina tatizo, niliwekwa ndani siku niliyopata ajali lakini nilitoka kesho yake,”alisema.

“Nafahamu wenzangu wanaanza mazoezi kesho (leo jumatatu) lakini nitashindwa kujiunga nao kwasababu natakiwa kuripoti katika kituo cha polisi kama sheria zinavyosema na ndio maana nipo hapa Moro,” alisema.

Busungu alikuwa nje kwa muda mrefu ambapo ilisemekana aliondoka kikosini Yanga baada ya kutokuwa na mawasiliano mazuri na mmoja mabosi wa benchi la ufundi lakini ilidaiwa kuwa anarudi baada ya benchi la ufundi kubadilika.