Blagnon: Mbao msiwachezee kabisa

Muktasari:

Blagnon alisema kupata ushindi ni raha sana, lakini furaha kubwa ni pale timu inapofanikiwa kuchukua ubingwa wa mashindano husika na kuweka wazi kuwa kuifunga Mbao lazima ufanye kazi ya ziada.

STRAIKA wa Simba, Muivory Coast Fredrick Blagnon ambaye ameifunga Mbao Fc mara tatu amesema kwamba, kuifunga timu hiyo ni lazima utumie akili nyingi.

Blagnon amewafunga Mbao katika mechi mbili za ligi kuu akitokea benchi pamoja na mechi ya Fainali ya Kombe la FA ambapo, aliingia kuchukua nafasi ya Said Ndemla na kufunga bao la kwanza.

Akizungumza na Mwanaspoti, Blagnon alisema kupata ushindi ni raha sana, lakini furaha kubwa ni pale timu inapofanikiwa kuchukua ubingwa wa mashindano husika na kuweka wazi kuwa kuifunga Mbao lazima ufanye kazi ya ziada.

Blagnon alisema kuwa amefurahi kuwa miongoni mwa wachezaji waliochangia kuipa Simba ubingwa ingawa, mechi hiyo ilikuwa ngumu kwao kwani walikutana na timu bora ambayo imewasumbua mabingwa wa ligi, Yanga.

“Ukicheza na Mbao lazima utumie akili na uusome kwanza mchezo, Mbao ni timu nzuri sana na itakuja kufanikiwa zaidi hapo baadaye, nafanikiwa kuwafunga kwa sababu nakuwa nimesoma mchezo wao maana naanzia benchi hivyo najua uchezaji wao na mbinu za kutumia.

“Ijulikane kwamba tumecheza na timu bora, ilifanikiwa kuwavua ubingwa Yanga kwenye kuchuano hii na kuwafunga tena mechi ya mwisho na hata sisi tunapokutana nao tunatumia nguvu nyingi kuwafunga maana sio timu inayofungika kirahisi.

Namshukuru Mungu tumefanikiwa kuwafunga maana tumetimiza lengo letu,” alisema Blagnon.