Azam kwa Mbabane Swallows Kombe la Shirikisho Afrika

Muktasari:

Waswaziland wamefanikiwa kucheza na Azam baada ya kuwatoa Orapa United ya Botswana kwa mikwaju ya penalti 3-2 katika mchezo wa marudiano wa raundi ya awali uliofanyika kwenye Uwanja wa Mbabane nchini Swaziland.

Dar es Salaam. Mabingwa wa Kombe la Mapinduzi, Azam itaanza kampeni yake katika Kombe la Shirikisho Afrika (CC), dhidi ya Mbabane Swallows ya Swaziland katika mchezo wa raundi ya kwanza utakaofanyika mwezi ujao.


Waswaziland wamefanikiwa kucheza na Azam baada ya kuwatoa Orapa United ya Botswana kwa mikwaju ya penalti 3-2 katika mchezo wa marudiano wa raundi ya awali uliofanyika kwenye Uwanja wa Mbabane nchini Swaziland.


Mechi hiyo ililazimika kwenda kwenye penalti baada ya dakika 90 kumalizika kwa timu hizo kuwa sare ya bao 1-1 kutokana na kila timu kushinda ugenini, Mbabane ikishinda 1-0 nchini Botswana kabla ya jana jioni nao kupigwa 1-0.
Azam FC iliyojiwekea malengo ya kufika hatua ya makundi ya mashindano hayo mwaka huu, itaanzia  nyumbani (Azam Complex) Machi 12 mwaka huu na kumalizia ugenini kati ya Machi 17,18 na 19.


Mshindi wa jumla wa mchezo huo, atasonga mbele kwa hatua ya mwisho ya mtoano na kukutana na moja kati ya timu 16 zitakazokuwa zimetolewa kwenye raundi ya kwanza ya Ligi ya Mabingwa Afrika, mechi za kwanza zikifanyika kati ya Aprili 7, 8 na 9 na zile za pili zikipigwa kati ya Aprili 14, 15 na 16.


Timu zote zitakazopenya hapo, moja kwa moja zitakuwa zimeingia hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika, ambapo safari hii kwa mara ya kwanza zitapenya timu 16 badala ya nane, zitakazogawanywa katika makundi manne.