Azam, Mtibwa kuumana leo Kombe la FA

Muktasari:

Kocha msaidizi wa Azam, Iddi Cheche anasema wamejiandaa vizuri kuhakikisha wanashinda mchezo huo na kutinga robo fainali.

Dar es Salam. Hatua ya 16 bora ya Kombe la Shirikisho (FA) inaendelea leo kwa Azam kuikaribisha Mtibwa Sugar wakati Ndanda itakuwa ugenini Songea kuikabili Mighty Elephant.
Mechi nyingine leo itakuwa kati ya JKT Ruvu dhidi Madini kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid Arusha.
Kocha msaidizi wa Azam, Iddi Cheche anasema wamejiandaa vizuri kuhakikisha wanashinda mchezo huo na kutinga robo fainali.
"Tumejiandaa vizuri, najua tunakutana na timu ngumu na nzuri lakini malengo yetu ni kuingia robo fainali ya mashindano haya. Hivyo lazima tupambane tushinde," anasema Cheche.
Kocha msaidizi wa Mtibwa Sugar, Zubery Katwila alisema wako vizuri tayari kwa mchezo huo na malengo yao msimu huu kuhakikisha wanafika fainali na wanatwaa ubingwa.
"Malengo yetu ni kufika fainali na huwezi kufika huko bila kufika kwanza robo fainali halafu nusu. Sasa tunataka tuifunge Azam. Tunajua ni timu kubwa na itakuwa kwenye uwanja wao lakini tumejiandaa kuwashangaza."alisema Katwila.
Huko Songea, Ndanda imejipanga kufanya vizuri katika mashindano hayo kama ilivyokuwa mwaka jana, lakini kocha wa kikosi hicho Meja mstaafu Abdul Mingange amesema wataingia katika mchezo kwa tahadhali dhidi ya Mighty Elephant.
Mingange alisema licha ya kwamba tangu wamefika mvua imeendelea kunyesha na kukiwa na baridi kali lakini amejiandaa vizuri kwa mchezo huo.
"Hatuijui hiyo timu tunayokutana nayo kesho (leo) lakini kama iko katika mashindano haya basi ni nzuri hivyo tutacheza kufa na kupona kuhakikisha tunashinda mchezo huo na kwenda hatua inayofuata"alisema Mingange.
Kocha wa JKT Ruvu, Bakari Shime amesema wako tayari kwa mchezo dhidi ya Madini ingawa anajua utakuwa mchezo mgumu kutokana na ubora wa wapinzani wao.
xxxxxxxx