Atupele ala kiapo JKT Ruvu

Muktasari:

JKT ina pointi 20 baada ya mechi 24, lakini hilo halimtishi Atupele ambaye alisema watapambana mpaka dakika za mwisho wa ligi hiyo ili wanusurike kushuka daraja.

STRAIKA wa JKT Ruvu, Atupele Green, amekula kiapo jeshini akidai kuwa licha ya timu yao kuwa katika hali mbaya mkiani mwa msimamo wa Ligi kuu Bara, lakini katu haitashuka daraja.

JKT ina pointi 20 baada ya mechi 24, lakini hilo halimtishi Atupele ambaye alisema watapambana mpaka dakika za mwisho wa ligi hiyo ili wanusurike kushuka daraja.

Maafande hao wanapigana kikumbo na Majimaji yenye pointi 22, Toto Africans iliyo na pointi 25 na African Lyon yenye pointi 26.

Kila moja ya timu hizo katika kuepuka kushuka daraja, inamwombea mabaya mwenzake apoteze mechi na yeye ashinde.

Atupele alisema kuwa ni kweli JKT wapo pabaya, lakini hawatakubali ishuke daraja, huku akifichua kuwa ameshindwa kutikisa nyavu mara nyingi msimu huu ambapo ana mabao manne kwa sababu ya changamoto za msimu huu.

“Ni mapema sana mtu akisema tunashuka msimu huu kwa sababu bado kuna mechi sita mbele yetu ambazo tunaweza kufanya lolote,” alisema.

“Unajua katika soka mpira unadunda na mambo yanaweza kubadilika muda wowote, kwa hiyo mashabiki na wapenzi wa timu wapunguze presha kwetu.

“Changamoto hizi ambazo huwa zinatokea katika mpira na sio kwamba mimi nimeridhika, ila kikubwa ni upepo mbaya tu ulipita, katika soka hii hali popote ipo, ila nimejipanga kurudi upya katika mechi zilizobaki hizi.

“Mashabiki watulie, sisi na kocha tunafanya jitihada ili kuweza kuondokana na balaa la kushuka daraja.”