Ajib siyo wa masihara nyie

Muktasari:

Ajib ana mabao sita katika msimamo wa wafungaji bora wakati kinara, Simon Msuva ana 12. Alifunga mara ya mwisho katika mchezo wao wa mwisho dhidi ya Tanzania Prisons.

KOCHA Mkuu wa Simba, Mcameroon Joseph Omog ameweka wazi, Ibrahim Ajib siyo straika asilia kwa sababu anabadilika na mzuri zaidi anapocheza nyumba ya mshambuliaji wa kwanza.

Ajib ana mabao sita katika msimamo wa wafungaji bora wakati kinara, Simon Msuva ana 12. Alifunga mara ya mwisho katika mchezo wao wa mwisho dhidi ya Tanzania Prisons.

Akitolea ufafanuzi wa mchezaji huyo, Mcameroon huyo alisema: “Mbali na kufunga, Ajib ana msaada mkubwa katika timu kwa sababu anabadilika kiuchezaji na kwa tafsiri siyo straika wa moja kwa moja, ni mzuri anapocheza nyuma ya straika wa kwanza yaani namba 10 kwa sababu ana vitu vingi.”

“Ana uwezo wa kuchezesha timu na kutengeneza mawasiliano mazuri mbele na nyuma timu ikapata ushindi,” alisema Omog ambaye ndiyo kocha aliyewapa Azam FC ubingwa pekee wa Ligi Kuu mwaka 2013.

Wadau na wapenzi wa soka Tanzania wanamtambua Ajib kutokana na uwezo wake katika kumiliki mpira, kuchezesha timu na kufunga na Ulaya unaweza kumfananisha na Mjerumani wa Arsenal, Mesut Ozil.

 

OMOG AUMWA MALARIA

Katika hatua nyingine, Simba jana Ijumaa walianza mazoezi rasmi Uwanja wa Polisi ikiwa ni sehemu ya harakati zao za kuwania ubingwa wa Ligi Kuu na Jumatatu hii wanatarajia kuanza safari ya kwenda Kanda ya Ziwa. Lakini kocha wao tangu walipotoka kwenye ziara ya Dodoma, Arusha na Manyara, amekuwa akisumbuliwa na ugonjwa wa malaria. “Nilipata malaria kidogo lakini sasa hali yangu inaendelea vizuri na Ijumaa tutaanza mazoezi yetu rasmi kujiandaa na mechi sita za ligi zilizobaki, tunataka kufanya vizuri bila kupoteza hata moja,”alisema Omog.

“Nafikiri Jumatatu tutaanza safari kwenda Kagera,” alisema.