320 kushiriki Tanga Marathon 2017

Friday April 14 2017

By BURHANI YAKUB, TANGA

WANARIADHA 320 kutoka mikoa ya Tanzania Bara na Zanzibar wanatarajiwa kuchuana kwenye mbio za Tanga City Marathon 2017 zitakazofanyika kesho Jumamosi jijini hapa.

Mratibu wa mashindano hayo, Juma Mwajasho, alisema jana kuwa waliothibitisha tayari wamewasili jijini Tanga kushiriki mbio hizo ambazo mgeni rasmi atakuwa Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Martine Shigela.

“Hatukutegemea kama  kungekuwa na mwamko kama huu, tunashukuru mpaka sasa wakimbiaji 320 wamesharipoti tayari kuonyeshana kazi Jumamosi,” alisema.

Kwa mujibu wa wadhamini wa mbio hizo, kupitia meneja wao, Kawkab Hussein mashindano hato yamegharimu kiasi cha Sh20 milioni na zitakuwa na umbali wa  kilomita 42  ambapo mshindi atajinyakulia kitita cha Sh1 Milioni huku wa pili  akizoa Sh700,000 na wa tatu Sh500,000.

Pia kutakuwa na mbio za kilomita 10 ana mshindi wake atajinyakulia Sh700,000, wa pili Sh500,000 na wa tatu Sh300,000.