Mavugo ndio mpango mzima

Muktasari:

Mavugo ambaye ameweka historia ya kufunga mabao katika mechi sita mfululizo za Ligi Kuu pamoja na FA na kuwahakikishia wadau na mashabiki wa Simba wasiwe na wasiwasi mechi sita walizobakiwa nazo kwa sababu lazima kitaeleweka alisema.

KOCHA wa Simba, Mcameroon Joseph Omog amemsifu straika, Mrundi Laudit Mavugo ni mpambanaji na hakubali kushindwa ndiyo maana anafanikiwa na mchezaji mwenyewe amekazia, ikitokea anatoka uwanjani bila kufunga au wamepoteza ujue halali siku hiyo.

Mavugo ambaye ameweka historia ya kufunga mabao katika mechi sita mfululizo za Ligi Kuu pamoja na FA na kuwahakikishia wadau na mashabiki wa Simba wasiwe na wasiwasi mechi sita walizobakiwa nazo kwa sababu lazima kitaeleweka alisema.

“Kama watu wangekuwa wanajua moyoni, huwa naumia ikitokea natoka uwanjani bila kufunga bao au Simba imepoteza wasingekuwa wanazungumza kitu, huwa nakosa usingizi kabisa ingawa wakati mwingine inabidi nikubaliane changamoto zao ili nifanye vizuri zaidi,”alisema Mavugo anayeweka wazi kuzoea hali ya hewa na mazingira ya Tanzania ndiyo yanamfanya ang’are.

Kuhusu kiwango chake, Mavugo amesema: “Hata hivyo, kiwango changu sasa ndiyo kinaanza kuonekana kwa sababu wakati nacheza kwetu Burundi nilikuwa nafunga mabao mengi na ni mchezaji mkubwa.”

“Nilikuwa katika wakati mgumu mwanzoni wakati nakaa benchi au nikipata nafasi mambo yanakuwa magumu sifungi, nilikuwa naumia lakini sasa nimezoea mambo yatakuwa mazuri.”

Akizungumzia mechi za ligi zilizobaki, Mavugo alisema: “Simba iko vizuri, binafsi sina wasiwasi na michezo hiyo tutafanya vizuri na Simba tutachukua ubingwa.”

Katika mechi alizofunga mavugo ni pamoja na Majimaji, Polisi Dar es Salaam, Prisons, Mbeya City, Yanga pamoja na Madini, pia Simba itacheza na Kagera Sugar, Toto na Mbao ugenini na nyumbani watakipiga na Mwadui, Stand na African Lyon.