Simiyu yang’ara kitaifa ukuaji shule binafsi za Sekondari

Test

Muktasari:

Kwa mujibu wa takwimu za msingi za elimu kwa mwaka (BEST) 2015 zilizotolewa Septemba 2015, mkoa wa Simiyu umeshika nafasi ya kwanza ukiwa na ukuaji wa asilimia 67 ukifuatiwa na mkoa wa Katavi wenye asilimia 50.

Mwandishi Wetu, Mwananchi

Dar es Salaam.Shule za binafsi za sekondari zimeongezeka kwa kasi katika mikoa mpya wa Simiyu kutoka shule sita hadi kufikia shule 10 ikiwa ni ongezeko la zaidi ya nusu ya shule hizo ndani ya mwaka mmoja.

Ongezeko hilo limeufanya mkoa wa Simiyu kuwa wa kwanza kitaifa katika ukuaji wa shule za Sekondari binafsi nchini  na kuzidi kutoa matumaini mapya ya kukua katika sekta ya elimu siku zijazo.

Kwa mujibu wa takwimu za msingi za elimu kwa mwaka (BEST) 2015 zilizotolewa Septemba 2015, mkoa wa Katavi umeshika nafasi ya pili ukiwa na ukuaji wa asilimia 50.

Katika takwimu hizo, Shinyanga imeshika nafasi ya tatu kwa kuwa na ongezeko la shule binafsi tano (asilimia 47.1) mpya kwa kila kumi zilizopo mkoani hapo.

Wakati mikoa ya Simiyu,Katavi na Shinyanga ikichangamkia fursa ya kuwa na shule za binafsi ili kukidhi mahitaji ya elimu yanayokuwa kwa kasi, hali imekuwa tofauti katika mikoa ya Arusha na Kagera ambayo shule nyingi zimekufa..

Takwimu hizo zinaonyesha kuwa shule 16 sawa na asilimia 20 mkoani Arusha ikifuatiwa na mkoa wa Kagera ambao asilimia mbili ya shule hizo zilikufa kutokana na sababu mbalimbali.