Kocha wa Massau Bwire kaanza mambo jamani

Muktasari:

Malale, ambaye amerithi mikoba ya Selemani Mtingwe aliyetimuliwa, alisema; “Nipo na timu sio muda mwingi sana, kwa kifupi haiko vibaya lakini nimegundua kuwa kuna mapungufu katika sehemu tatu muhimu ambazo ni kipa, kiungo na straika na nimeshawafahamisha mabosi juu hali hiyo.”

KOCHA mpya wa Ruvu Shooting, Malale Hamsini amekitazama kikosi cha timu hiyo kwa makini na kufichua siri kuwa kama mabosi wake watampa pesa basi mambo yake yatakwenda sawa katika mzunguko wa pili wa Ligi Kuu Bara kwa kuwa ataongeza watu wa shoka watupu kikosini.

Malale, ambaye amerithi mikoba ya Selemani Mtingwe aliyetimuliwa, alisema; “Nipo na timu sio muda mwingi sana, kwa kifupi haiko vibaya lakini nimegundua kuwa kuna mapungufu katika sehemu tatu muhimu ambazo ni kipa, kiungo na straika na nimeshawafahamisha mabosi juu hali hiyo.”

Kocha huyo, ambaye alisitishiwa ajira yake katika kikosi cha JKT Ruvu kabla ya kujiunga na Shooting aliongeza; “Katika kuandaa timu ili iwe na ushindani nimeona ni vizuri kwa siku tuwe tunafanya mazoezi mara mbili, yaani asubuhi na jioni ili kujenga timu iliyokuwa imara na yenye ushindani. Ligi ni ngumu sana na kila timu inataka kupambana kufikia malengo waliyojiwekea, ambayo ni kubeba ubingwa.”

Ruvu ambayo msemaji wao ni Massau Bwire, ipo katika nafasi ya tisa na pointi 19, lakini inapambana kuondoka kabisa katika eneo la kushuka daraja baada ya kufanya uzembe na kushuka daraja mwaka jana kabla ya kupanda tena jambo ambalo hawataki lijitokeze tena hivyo, wanapambana kwelikweli.