Mkwasa, mpango bomba ila..

Muktasari:

Ni sawa wazo hilo kuanza kujadiliwa ngazi hiyo ya juu lakini utekelezaji wake unapaswa kuanzia chini kwenye msingi ambao, ni vituo vya shule za soka na hata zile za elimu ya kawaida kisha timu za madaraja ya chini na hivyo ndivyo unavyoweza kudhani siku moja Tanzania inaweza kujenga aina yake ya soka kama ilivyo kwa nchi za Ulaya na Amerika ya Kusini zilizofanikiwa kubuni aina ya soka ambalo bado linaendelea kuwa nembo ya nchi hizo.

HIVI karibuni amesikika Kocha Mkuu wa timu ya Taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’, Charles Boniface Mkwasa, akiitaka TFF imuandalie mkutano na makocha wa timu za Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) Bara.
Moja ya ajenda ikiwa ni kujadili uwezekano wa kubuni aina na staili ya soka ambalo litajulikana kama ‘Soka la Kitanzania’ yaani (football made in Tanzania).
Nianze kwa kumpongeza Mkwasa kwa fikra na rai yake hiyo ambayo kwa mtazamo wangu inawezekana na si yeye pekee alikuwa na wazo hilo, lakini amekuwa wa kwanza kuliweka hadharani ili lijadiliwe na makocha wenzake na isiwe hao wa Ligi Kuu tu kwani, soka halijengwi kuanzia ngazi hiyo.
Ni sawa wazo hilo kuanza kujadiliwa ngazi hiyo ya juu lakini utekelezaji wake unapaswa kuanzia chini kwenye msingi ambao, ni vituo vya shule za soka na hata zile za elimu ya kawaida kisha timu za madaraja ya chini na hivyo ndivyo unavyoweza kudhani siku moja Tanzania inaweza kujenga aina yake ya soka kama ilivyo kwa nchi za Ulaya na Amerika ya Kusini zilizofanikiwa kubuni aina ya soka ambalo bado linaendelea kuwa nembo ya nchi hizo.
Historia ya soka inatukumbusha baadhi ya nchi zilizofanya vema katika hili, Italia ikiwa ni miongoni mwao ilipoamua kulijenga soka lake kwa mfumo wa kuzuia au kujihami zaidi. Staili yao hiyo waliita Catenaccio, neno hili kwa lugha yao ya Kitaliano linamaanisha ‘Kufuli’ yaani lango linafungwa kwa kufuli na si kuegesha tu, ni kuhakikisha hakuna kinachopenya kuingia langoni mwao.
Aina hii ya kuzuia na watu zaidi ya wanane wakiwa wote nyuma ya mpira inafanana sana na kile kinachoitwa kwa sasa “kupaki basi.”
Kwa Wataliano mpira unapaswa kuchezwa mbele kwenye lango la adui, hivyo ndivyo ilivyo hadi miaka ya karibuni ilikuwa bado vigumu timu za Italia kupoteza mchezo kwa bao zaidi ya moja.
Pamoja na mabadiliko, kwa sasa bado Wataliano hawachezi pasi nyingi kwenye eneo lao, na kwa upande mwingine wanaanza kukaba kwa nguvu kwenye eneo la adui ili kuinyima timu pinzani nafasi ya kulikaribia lango lao, hivyo kufanya mechi zao nyingi kuwa ngumu na sare kutawala huku tegemeo likiwa uwezo binafsi wa washambuliaji na kufanya penalti ziamue matokeo ya michezo yao iliyo mingi na hata zile fainali za Ulaya na Kombe la Dunia.
Hili ndilo soka la Kiitaliano linalohitaji nguvu, jihadi wakati mwingine hata rafu kuhakikisha kufuli limefunga kwelikweli.
Unapowaangalia Wahispania kama nchi na hata timu zao kubwa za ligi, pamoja na kukaribisha wachezaji nyota kutoka nchi nyingi bado soka lao ni lile lile linalozingatia maana halisi ya mchezo wenyewe kama unavyojulikana (Team Sport), soka ni mchezo wa kitimu zaidi unaohitaji ushirikiano ndani na nje ya uwanja na wachezaji wanapaswa kupasiana mpira kwa uhakika zaidi na kipaumbele kwao ni ufundi wa kuuchezea mpira, kufungua nafasi haraka kisha kupasiana na kulishambulia lango la timu pinzani kwa pamoja kwa haraka zaidi. Kadhalika kujilinda kwa kunyang’anya mpira kwa haraka sana.
Hivyo kuutunza mpira ndilo jambo muhimu kwao. Hii ni staili bora na inaimarishwa na mafunzo ya msingi ya kuumiliki mpira kuanzia katika akademi na vituo vya soka nchi nzima.
Ndio sababu timu zote Hispania zinacheza soka la aina moja tofauti kidogo inaletwa na uwezo binafsi wa wachezaji mfano Barcelona na Real Madrid zinatawala kutokana na uwezo binafsi wa kina Lionel Messi, Luis Suarez, Neymar na Cristano Ronaldo na Gareth Bale.
Na hata huko nyuma thamani ya kina Samuel Eto’o, Ronaldinho ilileta tofauti Barcelona na pale Madrid ni kina, Benzema na Bale, ndiyo wanaoleta tofauti lakini unapoziangalia timu hizi zikipambana na timu ndogo bado huwezi kuona tofauti kiuchezaji na ndivyo ilivyo timu ya taifa ya Hispania, inacheza ili kushinda na kuburudisha.
Hata hivyo, kwa Afrika Mashariki hususan Tanzania, bado haya hayajaonekana hasa katika timu za taifa unaweza kuitaja Kenya pekee ambayo siku zote tangu enzi za Kombe la Gossage ilifahamika kwa mchezo wa kutumia nguvu nyingi unaoendana na maumbile makubwa kisha kubuni staili ya pasi chache na kupiga mipira mirefu ya juu iliyotumiwa vizuri na washambuliaji wake warefu na wenye nguvu kuwapatia mabao.
Nchi nyingine za Afrika kama Ghana iliyotawala soka la Afrika miaka ya mwanzo ya nchi za bara hili kujikomboa kutoka kwa wakoloni ilicheza soka la aina yake likitegemea pasi na uwezo binafsi wa wachezaji enzi hizo kina Osei Koffi, Kwasi Ousu, Odam Clifford.
Na wakati huu unapoiangalia Ghana mchezo wake bado ni aina ileile, pasi tano hadi nane kabla ya shambulizi la mwisho.
Ni vyema watu wafahamu kuwa staili ya uchezaji ni tofauti na mfumo wa uchezaji mfano 4:2:4 au 4:5:1 mbali na hiyo mfumo na staili unaamuliwa na aina ya wachezaji na utamaduni wa nchi husika.
Nchi yenye watu wenye miili mikubwa kama Kenya mfumo hauwabadilishi wakaacha kutumia nguvu kama jadi yao.  Hivyo ndivyo unavyoweza kutegemea kwa nchi ya Brazil hata ingekuwa na maumbile makubwa kiasi gani isingecheza kama Kenya au Italia,  itapenda kucheza samba siku zote kama inayoendana na utamaduni wa watu wa nchi hiyo.
Uholanzi siku zote itacheza kitu kinachoitwa “Total Football”, wanazuia na kushambulia pamoja. Msingi wa aina ya mchezo huo ni ufundi unaojengwa kupitia mpango bora wa maendeleo ya soka la vijana chini ya KNVB nchi nzima kwa kufundisha soka halisi kuanzia watoto umri chini ya miaka sita kisha kusisitiziwa mwendo wa kasi uwanjani na ndivyo utakavyoiona timu ya taifa ya Uholanzi (The Orange) na hata klabu zao soka lao ni la ufundi mwingi na kasi huku wakizuia na kushambulia pamoja.
Baada ya hiyo mifano sasa tujadili wazo la Mkwasa; hivi kweli Tanzania tuna uwezo wa kubuni staili yetu ya uchezaji? Nasema inawezekana lakini napata wasiwasi malengo haya kufikiwa kwa kipindi kifupi kwani, jambo hili linahitaji maandalizi makubwa kujenga mwelekeo wa fikra (field behavior) ya wachezaji wetu ambao tayari wapo wengi wenye mapenzi na staili ya Kijerumani wengine wakishabikia soka la Hispania, Uingereza ambao soka lao halina ufundi mwingi isipokuwa nguvu na uwezo binafsi.
Maandalizi yatapaswa kuanzia chini hatua kwa hatua kwani kwa timu za Ligi Kuu inaweza kuwa vigumu hasa pale anapokuwepo kocha toka nje (Professional) ambaye kaajiriwa ili ailetee timu yake mafanikio na tayari ana mipango, staili na mfumo wake wa uchezaji anaouamini, haitakuwa rahisi kwake kukubaliana na mpango huu.
Mkwasa anastahili pongezi kwa wazo lake nadhani ingekuwa bora na rahisi wazo lake hilo ambalo ni zuri likajaribiwa kwenye timu za Copa Coca-Cola na hata Serengeti Boys wakati likifanyiwa utafiti wa kina kwa utekelezaji, vinginevyo changamoto bado nyingi na inaweza kuwa ni upotevu wa rasilimali muda, watu na fedha iwapo litafanywa bila umakini.
Kwa ushauri tu kupitia uzoefu kutoka nchi mbalimbali na historia ya soka letu na la dunia, maumbile ya Watanzania walio wengi ambayo ni madogo, lakini wamejaaliwa ujanja, wepesi na ubunifu, inawezekana kuunda aina ya soka inayofanana kidogo na Ghana, pasi chache nyuma, pasi tatu katikati na pasi mbili hadi tatu kabla ya shambulizi la mwisho, mchezo huu ulenge kutogusana sana na wapinzani pia kujenga uwezo wa upigaji mashuti yanayolenga goli na umaliziaji mzuri. Zoezi ambalo hupuuzwa na makocha karibu wote kuanzia kwenye akademi.
Nimelipendekeza soka la Ghana kutokana na historia ya nyuma. soka la Tanzania kama taifa hata klabu siku za nyuma miaka ya 1960 lilifanana sana na la Ghana na hii ilithibitishwa na matokeo ya mechi kati ya Asante Kotoko ya Ghana na Yanga zilizoonyesha kucheza soka linaloshabihiana kila kitu, Kotoko pasi zao na aina ya ushambuliaji wa pasi saba hadi nane huku wakimtegemea Osei Koffi na ndivyo ilivyokuwa kwa Yanga pasi saba hadi nane ikimtegemea Maulid Dilunga kuipatia ushindi na hivyo ndivyo Taifa Stars na Black Stars walivyokuwa wakicheza pia.
Tutapaswa kujenga uwezo mkubwa wa kumiliki mpira kwanza ili kuweza kuyafikia malengo haya.