Mavugo kanoga Taifa, Kisiga katamba ugenini

Muktasari:

Hata hivyo, katika mchezo huo Ndanda iliweka rekodi mpya ya kuweza kufunga bao dhidi ya Simba baada ya kucheza dakika 360 dhidi ya mabingwa hao mara 18 wa Ligi Kuu bila kuwafunga bao hata la kuotea. Bao la dakika ya 37 la Mponda liliifanya Ndanda kuifunga Simba bao la kwanza baada ya kucheza dakika 396 dhidi yao ambapo pia imepoteza mechi zote hizo.

NDIYO hivyo tena, uhondo wa Ligi Kuu Bara umeanza. Kila mdau wa soka alikuwa akisubiri kwa hamu kuanza kwa msimu mpya wa Ligi Kuu Bara ambao juzi Jumamosi ulikata utepe kwa mechi za ufunguzi na jana Jumapili ilikuwa ikiendelea.
Ilikuwa ni wikiendi ya soka hasa ukitazama pia ligi mbalimbali duniani kama ya England, Hispania na Italia nazo zilikuwa hewani.
Jana Jumapili kwenye Ligi Kuu Bara kulikuwa na mechi mbili kati ya Kagera Sugar ya Mecky Maxime na Mbeya City ya Kinnah Phiri wakati ambapo Toto Africans ilikuwa wenyeji wa Mwadui ya Kahama lakini mechi nyingine tano zilichezwa juzi Jumamosi. Pengine ilikuwa ni Jumamosi yenye msisimko mkubwa.
Mwanaspoti linakuletea matukio makubwa ambayo yametokea wikiendi ya kwanza kabisa ya Ligi Kuu Bara.

Bao la mapema, usiku
Subianka Lambert wa Prisons ya Mbeya aliifungia timu yake bao katika dakika ya nane na kuipa ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Majimaji mjini Songea. Prisons ilianza kampeni yake vizuri chini ya kocha mpya Meja mstaafu Abdul Mingange, lakini gumzo kubwa linabaki katika bao la Lambert ambayo ndilo lililofungwa mapema zaidi wikiendi hii (kabla ya mechi za jana).
Nahodha wa Azam, John Bocco anaingia kwenye gumzo la wikiendi pia akiwa ni straika aliyefunga bao la usiku zaidi. Bocco aliifungia Azam bao la kusawazisha dhidi ya African Lyon katika dakika ya 90+3 na kuisaidia timu yake kupata angalau pointi moja katika mchezo wa ufunguzi.

Ushindi mkubwa
Mabingwa wa zamani wa Ligi Kuu, Simba imekuwa timu pekee iliyoanza msimu kwa karamu ya mabao baada ya kuifunga Ndanda FC ya Mtwara kwa mabao 3-1. Shukrani kwa mabao ya Laudit Mavugo, Blagnon Frederick na Shiza Kichuya ambayo yaliifanya Ndanda kukosa pointi kwenye Uwanja wa Taifa licha ya Omary Mponda kuifungia Ndanda bao la kufutia machozi.
Hata hivyo, katika mchezo huo Ndanda iliweka rekodi mpya ya kuweza kufunga bao dhidi ya Simba baada ya kucheza dakika 360 dhidi ya mabingwa hao mara 18 wa Ligi Kuu bila kuwafunga bao hata la kuotea. Bao la dakika ya 37 la Mponda liliifanya Ndanda kuifunga Simba bao la kwanza baada ya kucheza dakika 396 dhidi yao ambapo pia imepoteza mechi zote hizo.

Kadi nane za njano
Ibrahim Ajib wa Simba alipewa kadi ya njano baada ya kutaka kumdanganya mwamuzi kuwa amechezewa madhambi ndani ya eneo la hatari ili kupata penalti lakini hadi siku ya Jumamosi inamalizika jumla ya nyota wanane walipewa kadi za njano. Aziz Sibo alipewa kadi ya njano pia katika mchezo huo dhidi ya Simba. Nyota wengine waliopewa kadi za njano ni Revocatus Richard, Abaslim Chidebele na Miraji Maka wa Stand United, Leons Mutalemwa na Victor Hangaya wa Prisons pamoja na Alex Kondo wa Majimaji ya Songea.

Mayanga rekodi mbovu
Kocha wa Mtibwa Sugar, Salum Mayanga ameendeleza rekodi yake mbovu ya mechi za ufunguzi wa Ligi Kuu Bara baada ya kufungwa bao 1-0 na Ruvu Shooting nyumbani. Bao pekee la Shaaban Kisiga liliipa Ruvu ushindi muhimu wa kwanza Ligi Kuu, lakini likaongeza machungu kwa Mayanga ambaye sasa ataendelea kusubiri kupata ushindi katika mechi yake ya kwanza msimu ujao. Msimu uliopita akiwa na Prisons, Mayanga alipoteza pia mchezo wa kwanza kwa kipigo cha mabao 2-1 kutoka Azam.

Waliopanda wakaza
Timu zote tatu zilizopanda kushiriki Ligi Kuu kwa mara ya kwanza msimu huu hazikupoteza mechi zao za ufunguzi jambo ambao limetoa ishara ya msimu mgumu. Ukiachana na Ruvu Shooting ambayo ilikuwa timu pekee iliyopanda daraja kushinda mchezo wa ufunguzi, Mbao FC iliibana mbavu Stand United wakati African Lyon ilipata sare dhidi ya Azam. Uzuri ni kwamba timu zote hizi zimepata matokeo hayo ugenini.

Kisiga, Kichuya kuchuana
Mabao yaliyofungwa na Shaaban Kisiga na Shiza Kichuya huenda yakawa ndiyo mabao bora zaidi katika wikiendi ya kwanza ya Ligi Kuu japokuwa mjadala mkubwa unaweza kubaki kuwa bao lipi ni bora zaidi. Kisiga alifunga bao kwa mpira wa adhabu ndogo nje kidogo ya eneo la hatari na kufanya mwendelezo wa kufunga mabao ya aina hiyo. Kichuya alifunga bao kwa shuti kali la moja kwa moja nje kidogo ya eneo la hatari akirejesha mpira uliokuwa umeokolewa na mabeki wa Ndanda. Pengine bao la Kichuya linaweza kuwa na alama nyingi zaidi kutokana na namna lilivyofungwa. Lakini bao lililokuwa gumzo katika mechi za ufunguzi ni lile la Hood Mayanja wa African Lyon aliyepiga kona iliyoenda moja kwa moja wavuni mwa lango la Azam, kitu ambacho kwa miaka mingi hakijawahi kutokea katika VPL.

Mabao yasubiriwa
Mechi za jana Jumapili zitatoa takwimu halisi ya mabao ya mechi za ufunguzi Ligi Kuu kwani pamoja na mabao manane kufungwa Jumamosi bado kuna uwezekano wa mabao mengi zaidi kupatikana. Jana Mbeya City ilisafiri kuifuata Kagera Sugar huku Toto Africans ilikuwa wenyeji wa Mwadui ya Kahama. Mchezo wa kiporo baina ya Yanga na JKT Ruvu utachezwa mwishoni mwa mwezi huu na kukamilisha mechi za ufunguzi.