KAFARA LA KISHETANI-18

Muktasari:

Wakati nipo ndani ya gari sababu ya uchovu, niligeuka na kuangalia ile maiti ya mtoto nikagundua ilibadilika rangi na kuwa nyeusi ikionekana kutoka jasho. Mambo hayo sasa yakaanza kunitoa ujasiri.

ILIPOISHIA. Sikutaka kusimama, niliendesha gari mwendo wa kasi nikiamini ndoto zangu za kuwa bilionea mtoto zinaenda vema. Umbali wa mita chache niliona gari zikinifuata nyuma, sikutaka kujidanganya kama wasingeweza kunikamata kirahisi. Nilikatisha na kuikamata barabara ya Ali Hassani Mwinyi.
Tulipofika kwenye taa za barabarani njia panda ya kwenda Kinondoni taa ya njano ilionyesha kunitahadharisha kutopita kwani nyekundu ingefuata sekunde chache. Hilo kwangu sikulitia akilini, nilikatisha na kuingia upande wa pili nikihakikisha gari langu halipunguzi mwendo.
Bahati nzuri zile gari zilizokuwa zinanifuata zilikutana na taa nyekundu ambayo haikuwaruhusu hivyo kuniwezesha kufanikiwa kuwatoka kirahisi.
Pamoja na mambo yangu kwenda fresh hasa ukizingatia uchawi wa kitajiri niliofanya, moyoni bado nilikuwa na deni kubwa kwa wanangu wapendwa ambao walipoteza dira ya maisha na hatimaye kugeuka ndondocha. Kila nilipofikiria hilo lawama nilizipeleka kwa mke wangu aliyeniacha na kuchukuliwa na rafiki yangu wa karibu Raymond.
Endelea...
Sikujua hali yake, nilichotaka hakikuwa kingine zaidi ya utajiri. Baada ya mwendo mfupi gari langu lilianza kupungua upepo gurudumu la mbele kushoto.
“Sijui balaa gani hili,” nilijisemea nikifungua mlango na kufunga kutumia ‘rimoti’ kusudi mtu asiingie kirahisi.
“Ebwana, vipi braza...” alifika kijana mmoja baada ya kuegesha gari langu.
“Safi, gari imepata pancha...”
“Ngoja tukutengenezee chapchap!” Aliniambia, sikuwa na ujanja. Nilifungua buti na kutoa gurudumu la ziada pamoja na jeki, kijana huyo akaanza kazi. Nilikuwa mtu mwenye mawazo mengi, kila mara niliingia garini na kutoka bila kujua nilitaka kufanya jambo gani. Matukio mazito yaliniumiza moyoni licha ya kujifanya sijali. Kuua msichana mrembo, kuiba maiti ya mtoto mdogo hospitali na kuwafanya wanangu ndondocha huku nikifanya mapenzi na jini Maimuna na kulala kwenye jeneza vilikuwa vitu vya kimazingara.
Nilijua nimeingia katika ulimwengu wa shetani, huenda siku yangu ya kufa ningeteseka sana maana nilijiona katili na muuaji. Matendo yote haya yalinifanya niwe na roho ngumu isiyo na huruma.
Wakati nipo ndani ya gari sababu ya uchovu, niligeuka na kuangalia ile maiti ya mtoto nikagundua ilibadilika rangi na kuwa nyeusi ikionekana kutoka jasho. Mambo hayo sasa yakaanza kunitoa ujasiri.
“Duh! Maiti inatoa jasho na kubadilika rangi!” Nilibaki mwenye mawazo mengi.
Yule kijana alipomaliza, nilimlipa kiasi cha elfu tano kama shukurani na kuondoka. Dakika chache nilifika nyumbani na kukutana na kundi kubwa la watu. Sikujua nini kilitokea, niliegesha gari  hatua ishirini kutoka nyumba ninayoishi, nikafunga vema milango na kutembea kigoigoi.
Askari wengi walikuwepo, nilipowaona ndugu wa mke wangu nilisoma sura zao nikagundua walikuwa na huzuni na wanyonge. Haraka nikajiambia akilini huenda kipigo alichopata mke wangu baada ya kumtishia jini kilimtoa uhai baada ya kulazwa hospitali ya Amana Ilala.
“Vipi, kuna nini?” Niliuliza nikiangaza macho.
“Msiba!”
“Msiba wa nani?”
“Mtoto wa Bibi Mbago!”
“Kweli, yule msichana mzuri?”
“Ndiyo, amekufa katika mazingira ya ajabu...,” waliniambia, pale pale nilianza kuonyesha uso wa manjozi, ingawa moyoni nilifahamu kabisa ni katili.
Watu waliokusanyika walionekana wenye imani za dini, nyimbo mbalimbali za maombolezo ziliibwa, niliitikia nikionekana mwenye huzuni. Hata hivyo, nilichokiwaza akilini mwangu ilikuwa maiti ya mtoto. Nilifikiria jinsi gani ningeweza kuitoa maiti na kuingiza chumbani.
“Ndugu wa mke wangu wana uhusiano gani na msiba wa bibi Mbago?” Nilijiuliza akilini, muda mfupi akanifuata mwanaume mmoja na kuniambia twende kando tuongee faragha. Sikumbishia nilijua anataka kunipa umbea.Tulitembea mita chache tukasimama.
“Habari yako Kimaro...,” aliniamkia akiningalia kiudadisi.
“Safi?”
“Wazima nyumbani?”
“Wazima, sijui utokako!”
“Salama, kwanza kabisa napenda nijitambulishe...mimi ni kaka yake na aliyekuwa mkeo, Lightness...”
“Ahaaah! Karibu sana...”
“Nishakaribia!” aliniambia, lakini akionyesha uso wenye mambo mengi kichwani, alipokea simu yake akaongea na mtu nisiyemfahamu kisha akakata.
Hakuonekana mwenye tabasamu badala yake akionekana ana dukuduku.
“Sikiliza, Kimaro...tumekufuata kwako kwa ajili ya kuwachukua wajomba zetu, hatutaki masuala mengine...,” aliniambia. Sura yangu ikabadilika.
“Wewe una mamlaka gani ya kuwachukua wanangu, nimewasafirisha...,” nilisema niking’ata meno.
Bado nilisumbuliwa na mawazo mengi. Sikutaka watoto hao wachukuliwe kwani ningepoteza utajiri.
“Ahaa, sawa..tunaondoka ila tutarudi...,” alisema kwa hasira na kuondoka.
Kabla ya kutoka eneo hilo alisimama na kuongea na kundi la watu watano kisha wakaingia ndani ya gari na kuondoka.
Hofu iliyonipata haikuwa ndogo nikajua kwa vyovyote wangerejea jioni.
Kama kawaida yangu, niliingia ndani nikakumbana na harufu kali, maiti ya mwanamke niliyoileta jana yake usiku ilishaanza kutoa harufu kali, nilijikaza kiume na kutembea hadi nilipoilaza na kugundua tayari mwili wake ulianza kuvimba.
“Mbona balaa, hii maiti ikikaa mpaka kesho asubuhi lazima majirani watagundua, jambo la kufanya hapa ni kutafuta dawa za kufukiza,” niliwaza.
Sikuwa na raha, nilitembea na kutoa kichwa cha maiti kilichokuwa kwenye begi kubwa kisha nikatoka nalo nje nilipoegesha gari.
Sikutaka kupoteza muda, niliingiza maiti ya mtoto na kuipeleka chumbani.
Zikawa maiti mbili, tena zilizokuwa nyumba ya kupanga, ulikuwa mtihani mgumu sana, kwani nilifahamu kesho yake mambo yangekuwa mabaya zaidi.
Harufu ingekuwa mtindo mmoja na lazima askari wangefika kunipekua, kuna kinachotoa harufu kali.
Nikiwa chumbani, akatokea jini Maimuna, alikuwa amevaa ‘dira’ nguo fulani ndefu akionekana kunukia marashi, alipofika alinikumbatia akiniambia tayari nishakuwa bilionea.
“Kwa nini?”
“Umeweza, ukienda Kariakoo utakuta duka kubwa limefunguliwa na aliyefanya kazi hiyo ni mpenzio, sheria na sharti kubwa la kulinda utajiri huu, kamwe hutakiwi kuzini na mwanamke, mwanamume wa aina yoyote aliyehai.
Masharti mengine, utakuwa ukizini na maiti, ili kuongeza utajiri.
“Ahsante, kwa hiyo duka lipo kubwa?”
“Ndiyo, usihofu linauza si mchezo...,” aliniambia Jini Maimuna, nilidhani ananitania.
Niliingia ndani ya gari na kuanza safari ya kuelekea Kariakoo mtaa wa Kongo, hakika nilistaajabishwa na mambo niliyoyaona.
Duka lilikuwa limesheheni wateja, wauzaji wake walikuwa wasichana wazuri waliokuwa watupu!
Nilishangaa kuliko kawaida, niliwaona isipokuwa wateja hawakuona kinachoendelea, siri nzima niliihifadhi.
Waliuza nguo za kila aina, vipuri vya kinamama na bidhaa mbalimbali, lilikuwa duka kubwa ambalo halikupungua wateja.
“Maimuna..”
“Rabeka...”
“Hawa wasichana ni kina nani?”
“Huyu mmoja ni ile maiti ya mrembo....”
“Kweli!”
“Ndiyo...”
“Mwingine!”
“Mtoto wako wa kike, huyu kazi yake ni kuhifadhi pesa...”
“Loh! Ehee, na hiki kibabu chenye kutoa udenda!”
“Mwanao James...”
“Kweli, mbona miujiza...”
“Siyo miujiza, uchawi ni sayansi ya juu sana...lakini ukikosea masharti ndugu utateseka sana...”
“Siwezi kukiuka masharti...,” nilisema, nikaingia ndani ya duka na kuona minoti kibao, watu walinunua bidhaa.
Kiumbe aliyekuwa akienda kufunga mzigo alikuwa mpenzi wangu jini Maimuna. Kariakoo nzima, wengi walimwita Anti Cash, sababu ya utafutaji wake ingawa hakuna aliyeweza kugundua mke wangu huyu ni jini mwenye uwezo wa kuua na kula nyama za watu.
Jioni nilipiga mahesabu, nilikuwa nimepata milioni ishirini kutokana na mauzo ya jumla na rejareja, mpenzi wangu Maimuna aliniweka wazi kuwa nitakuwa bilionea ndani ya muda mfupi.
Sikuamini lakini wiki moja baadaye nilishafungua maduka matano na yote yalikuwa yakifanya vizuri.
Wale ndondocha wangu niliwagawanya na kila mmoja aliuza duka lake.
“Duka moja halina ndondocha...” Maimuna aliniambia.
“Kwa hiyo, nifanyeje?”
“Dawa ni kuongeza maiti moja...”
“Ya nani?” nilimuuliza.
“Mtu unayempenda sana...”
“Mke wangu...”
“Hapana, unanidanganya...Kimaro nataka maiti ya mtu unayempenda sana...”
“Maimuna, hapo pabaya....”
“Kwa nini?”
“Huyu mtu ninayempenda siwezi kumuua...”
“Basi, umeshindwa...”
“Sijashindwa, nipe mtihani mwingine...”
“Kwanza niambie unampenda nani?”
“Baba yangu na tayari alishakufa!”
“Sasa hivi?”
“Nampenda sana mama yangu mzazi...”
“Yupo wapi?”
“Rombo!”
“Sawa, unaweza kumleta mjini?”
“Kufanya nini, Maimuna usinitende...”
“Hapa nipo kazini, Jini Sultani anataka damu...”
“Ya nani?”
“Mama yako...”
“Siwezi, siwezi kutoa damu ya mama yangu, kama ni utajiri niukose...,” niliongea kwa ukali, Jini Maimuna akacheka sana na kuniambia najidanganya, damu ya mama yangu lazima nitaitoa tu, kwa njia nyingi.
“Njia gani?”
“Utajua siku moja!”
Maneno yake yalinifanya niuchukie utajiri na kutamani kurejea kwenye hali yangu ya maskini. Sikutaka kamwe nimwondoe mama yangu kipenzi, nilikuwa na kila sababu ya kutafuta pesa kwa ajili ya kumtunza mzazi wangu huyo ambaye umri wake ulidhohofika.
Baada ya kufurahia utajiri wa kichawi, niliingia ndani ya gari na safari ya kurejea nyumbani ilianza, sikuwa na furaha hata kidogo kila nilipokumbuka kuwa nilihitajika kumwaga damu ya mama yangu sababu tu ya pesa. Ni jambo ambalo kamwe sikutegemea kulifanya.