Yanga isichukulie poa, ilinde heshima kwa Mazembe

Muktasari:

Ushindi wa Yanga katika mechi hiyo utaijengea heshima klabu hiyo na Tanzania kwa jumla kwa hiyo haipaswi kuingia ikiwa imekata tamaa.

WAKATI pazia la Ligi Kuu ya Soka ya Tanzania Bara limefunguliwa, Yanga wana mtihani wa mwisho mbele yao wa kupambana na TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo kesho.
Mechi hiyo ni ya kukamilisha ratiba ya hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho baada ya Yanga kupata matokeo ambayo yamezima ndoto za kuingia nusu fainali.
Yanga yenye pointi nne baada ya mechi tano za michuano hiyo inapambana na Mazembe ambayo tayari imeingia nusu fainali ya michuano hiyo na inasubiri timu ya kuungana nayo kutoka Kundi A kati ya Medeama ya Ghana yenye pointi nane na MO Bejaia ya Algeria yenye pointi tano ambazo nazo zitachuana katika mechi ya mwisho.
Pamoja na kwamba Yanga haina nafasi ya kusonga mbele katika michuano hiyo, lakini pambano hilo ni muhimu kwani inapaswa kulinda heshima yake kwa kutokubali kufungwa kirahisi.
Mbali na kulinda heshima Yanga iwapo itashinda mechi hiyo na Mazembe, inaweza ikashika nafasi ya tatu katika msimamo wa Kundi A na kiasi cha fedha ambazo itapewa na Shirikisho la Soka la Afrika [CAF] kitaongezeka tofauti na ikishika nafasi ya mwisho kama ilivyo sasa.
Kwa mantiki hiyo Yanga haitakiwi kuhesabu pambano hilo kama la kukamilisha ratiba tu bali inapaswa ilichukulie kwa uzito mkubwa ili iweze kuongeza fedha itakazopata.
Kocha Mkuu wa Yanga, Hans Pluijm anapaswa kuweka sawa wachezaji wake ili wajione kuwa bado wapo kwenye mashindano na siyo kwamba, wanacheza mechi ambayo haina faida yoyote.
Ushindi wa Yanga katika mechi hiyo utaijengea heshima klabu hiyo na Tanzania kwa jumla kwa hiyo haipaswi kuingia ikiwa imekata tamaa.
Kwa upande mwengine safari hii Yanga itarudi kwenye Ligi Kuu Bara ikiwa na moto mkali kwani imepata maandalizi mazuri kwa ajili ya Ligi hiyo inayoshirikisha timu 16.
Mechi sita za Kimataifa ilizocheza katika hatua ya Makundi ya Kombe la Shirikisho ni maandalizi mazuri kwa ajili ya Ligi Kuu na hakuna timu nyengine yoyote iliyopata maandalizi kama hayo.
Ligi Kuu Bara ilianza mwishoni mwa wiki kwa kishindo na Yanga itakaporudi kwenye Ligi hiyo ukali na utamu utaongezeka na mwelekeo kuwa safari hii kutakuwa na patashika kubwa ya kupata bingwa.
Ligi hiyo imeanza kwa Kigogo Simba kupata ushindi wa mabao 3-1 dhidi ya Ndanda ya Mtwara kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam na huku Azam iliyoshika nafasi ya pili katika msimu uliopita ilitoka sare ya bao 1-1 na African Lyon katika Uwanja wa Azam Complex.
Mwanzo huo wa ligi kwa kuzingatia matokeo ya mechi hizo mbili inaonyesha kuwa ushindani utakuwa mkubwa kwani, timu zote zimejiandaa vyema.
Pamoja na Ndanda kufungwa na Simba lakini ilionyesha mchezo mzuri na siyo timu ya kubeza kwani kuna wakati iliibana Simba kabla ya Mabingwa hao wa zamani kutumia uzoefu wao kupata ushindi huo.
African Lyon ambayo imepanda daraja msimu huu ilikuwa inaiongoza kwa bao 1-0 Azam hadi dakika 90 na timu hiyo ya Chamazi ililazimika kusawazisha katika dakika za nyongeza maarufu kama dakika za majeruhi.
Kutokana na kasi iliyoonyeshwa katika mechi za ufunguzi za Ligi Kuu ni dhahiri kwamba, Yanga ambayo mashabiki wake wameipachika jina la wa kimataifa isije ikadhani katika Ligi Kuu kuna lele mama.
Hali inadhihirisha kuwa Ligi ya msimu huu itakuwa yenye ushindani mkubwa kwani kila timu inahitaji kufanya vyema na kujiweka vizuri katika msimamo wa ligi hiyo.
Japokuwa bado ni mapema kuweza kubaini hali halisi ya Ligi Kuu itakavyokuwa, lakini dalili zinaonyesha kuwa ligi ya msimu huu itakuwa na upinzani wa hali ya juu.
Jambo la muhimu ili ligi hiyo iwe bora na yenye ushindani wa kweli ni kwa waamuzi wanao chezesha ligi Kuu kuhakikisha kwamba, wanatoa maamuzi ya haki kwa kuzifuata vyema sharia 17 za mchezo wa soka ili bingwa atakayepatikana awe halali na afanye vizuri katika michuano ya kimataifa.
Pia ili ligi iwe na mashiko zaidi inabidi klabu ambazo zinaonekana kuwa za wastani zijitume bila kuogopa kwamba zinapambana na timu gani uwanjani.

Masoud Sanani ni Mwandishi wa Habari Mwandamizi amewahi kufanya kazi Televisheni Zanzibar, Uhuru na Mzalendo, Bussiness Times [Mhariri mwanzilishi wa Spoti Starehe] na Mwananchi. Alikuwa mkurugenzi wa Jukwaa la Wahariri Tanzania [TEF]. Anapatikana kwa email  [email protected]  simu 0712-020020