Wenger alivyojichelewesha kwa viungo hawa, kawakosa

Muktasari:

Arsene Wenger aliweka wazi kwamba amejipanga kuwekeza kwa kiungo wa kati matata kabisa Geoffrey Kondogbia na alikuwa tayari kutumia pesa ya kutosha kunasa saini ya mchezaji huyo.

KWA miaka kadhaa Arsenal bado inasumbuka kupata mchezaji kiungo mwenye makali ya kufikia kiwango cha Patrick Vieira alipokuwa akitamba kwenye kikosi hicho.
Kiungo wa kukaba ni eneo ambalo Kocha Arsene Wenger kwa muda mrefu amekuwa akisumbuka kumsaka mrithi sahihi baada ya kuondoka Vieira. Mwaka huu, Wenger amemnasa kiungo Granit Xhaka kwa ajili ya kuimarisha kwenye eneo hilo la kiungo.
Hata hivyo, kuna viungo kibao wenye uwezo mkubwa ambao Wenger angeweza kuwanasa na kuwaongeza kwenye timu yake ili kupata huduma nzuri, lakini alijichelewesha na kuwakosa.

Yaya Toure (2003)
Mdogo wake Kolo Toure, kiungo Yaya Toure alitaka kujiunga na Arsenal mwaka 2003, miaka miwili kabla ya Patrick Vieira kuachana na timu hiyo.
Hata hivyo, kibali cha kufanya kazi kilikuwa shida baada ya kiungo huyo Muivory Coast kufuzu majaribio yake kwenye kikosi hicho cha Kocha Arsene Wenger. Ikashindikana, akaondoka na kupita klabu mbalimbali kabla ya kutua Manchester City ambako amekuja kuitesa mara kadhaa Arsenal kutokana na kubeba ubingwa wa Ligi Kuu England zaidi ya mara moja.

Xabi Alonso (2008)
Dili la kumnasa kiungo Mhispaniola Xabi Alonso lilikuwa kwenye hatua za mwisho na mchezaji huyo alikuwa anaelekea kusaini kuichezea Arsenal mwaka 2008. Kocha wa Liverpool kwa wakati huo, Rafa Benitez alitaka kumpiga bei Alonso ili amchukue Gareth Barry. Alonso ni kiungo fundi wa mpira, lakini tatizo la Wenger hakutaka kutumia Pauni 18 milioni kuipata huduma ya mchezaji huyo na hivyo ni vyema awakuze tu Alex Song na Denilson.

Paul Pogba (2012)
Kiungo Mfaransa, Paul Pogba amerejea kwenye kikosi cha Manchester United kwa ada iliyoweka rekodi ya dunia kwenye uhamisho baada ya miaka minne tu kupita alipohama bure kwenda Juventus. Imekuwa rahisi Pogba kurudi kwenye Ligi Kuu England, lakini mambo yangekuwa tofauti kama angejiunga na Arsenal kipindi hicho wakati anaondoka Old Trafford. Kocha Wenger alikiri kwamba alitaka kumsajili kiungo huyo ambaye amemtaja kuwa ana kila kitu ndani ya uwanja, lakini alichelewa kufanya uamuzi na alipotaka kuchukua hatua tayari Pogba ameshakamilisha dili la kujiunga na Juventus.

Morgan Schneiderlin (2014)
Arsenal ilikuwa timu ya kwanza kabisa kuonyesha nia ya kumsajili kiungo Morgan Schneiderlin mwaka 2014, lakini Southampton waligoma kumuuza nyota wao mwingine wa kiwango kibwa hasa ikiwa tayari ilikuwa imewapoteza Luke Shaw aliyekwenda Man United na Adam Lallana na Dejan Lovren waliokuwa wamekwenda Liverpool mwaka huo. Mwaka uliofuata, Wenger alizidi kujichelewesha na Man United walishinda mbio za kumnasa Schneiderlin na kuiacha Arsenal ikiendelea kuwa na shida ile ile ya kukosa kiungo wa maana tangu alipoondoka Vieira.

Geoffrey Kondogbia (2015)
Arsene Wenger aliweka wazi kwamba amejipanga kuwekeza kwa kiungo wa kati matata kabisa Geoffrey Kondogbia na alikuwa tayari kutumia pesa ya kutosha kunasa saini ya mchezaji huyo. Hata hivyo, Wenger alichelewa tena na kushindwa kukamilisha dili na kiungo huyo alipoondoka AS Monaco akatimkia Inter Milan kwa ada ya Pauni 28 milioni. Kondogbia alikiri kwamba kocha Roberto Mancini ndiye aliyemshawishi kwenda Italia.

Sami Khedira (2015)
Wakati kiungo Mjerumani, Sami Khedira alipokuwa akiondoka Real Madrid tena kwa uhamisho wa bure kabisa, Arsenal ilikuwa na nafasi kubwa ya kumchukua mchezaji huyo na ingekuwa faida kubwa kwa timu hiyo kutokana na uzoefu wa mechi kubwa. Lakini, Wenger akaanza kuwaza mshahara ambao angemlipa kiungo huyo na hivyo kumfanya Khedira kuamua kutimkia Juventus, ambako ameendelea kuuwasha moto na juzi Jumamosi alipiga bao katika mechi ya kwanza ya msimu wa Serie A. Kwa mwaka jana, Arsenal ilimsajili kipa Petr Cech tu.

N’Golo Kante (2016)
Baada ya kufunguliwa kwa dirisha la uhamisho wa wachezaji tu mwaka huu, Arsene Wenger alionyesha waziwazi kuhitaji saini ya Mfaransa mwenzake, N’Golo Kante.
Kante alikuwa kwenye ubora mkubwa msimu uliopita alipokuwa na kikosi cha Leicester City na alikwenda kung’ara pia kwenye fainali za Euro 2016 na Wenger kuweka wazi kuwa ni aina ya kiungo ambaye angependa awemo kwenye timu yake. Lakini, kama kawaida yake, alichelewesha na Chelsea chini ya kocha wao mpya, Antonio Conte alipanda dau na kumnasa kiungo huyo kwa ada ya Pauni 30 milioni. Kuhusu Kante, Kocha Wenger hakumtaka tu safari hii, bali aliwahi kumfuatilia akiwa mdogo na aliacha akimsubiri akue kwanza.