Ajib ni mwanasoka aliyetoka Masaki?

Muktasari:

Kila nikimtazama Ajib anapocheza soka nahisi ni kama vile namtazama mchezaji ambaye nje ya uwanja ana kazi nyingine anazoweza kufanya kama vile kuwa Ofisa Benki, Mkuu wa Kitengo cha TRA au mfanyabiashara ambaye mambo yake yapo safi. Haonekani kuupania sana mpira. Anaudharau.

NAVUTIWA kumtazama mchezaji anayeitwa Ibrahim Ajib. Ukimtazama ndio unapata tafsiri halisi ya neno kipaji. Jinsi anavyokokota mpira, jinsi anavyonyambulika, jinsi anavyopiga pasi, jinsi anavyofunga mabao ya akili. Msimu uliopita bao lake moja lilichaguliwa kuwa bao la msimu.
Alikwenda katika sherehe za tuzo zilizochagua bao lake kuwa bora akiwa na suruali ya Jeans iliyochanwa makusudi na wabunifu wa nguo za kisasa.
Haikunishangaza sana. kila ninapomtazama Ajib huwa simwoni kama mtu makini sana.
Kwangu naamini kuwa kuna kitu anaweza kufanya zaidi, lakini Ajib huwa hafanyi. Kipaji chake kama kingechanganyika na wito wa kujituma kutoka moyoni nadhani Ajib angekuwa mbali sana. walio karibu naye wanasema Ajib hapendi mazoezi.
Walio karibu naye wanadai mazoezini kama kocha akiwaambia wachezaji wakimbie kwa kasi kwenda upande mwingine, wanaweza kumwacha Ajib akifunga kamba zake za viatu bila ya kumaliza. Anaamini soka ni kipaji pekee siyo mazoezi ya nguvu.
Hainishangazi sana kuona kwamba licha ya kipaji chake Ajib hana stamina. Akigusana bega kwa bega na mchezaji wa timu pinzani basi ataanguka chini na kujikung’uta jezi yake taratibu. Siyo mpambanaji. Bahati mbaya upambanaji hauanzii katika mechi, unaanzia mazoezini.
Kinachonisikitisha katika hili ni ukweli kwamba soka ndiyo maisha yake. Soka ndiyo kila kitu kwake. Kwa nini usimalizie kila kitu kwa kufanya juhudi kubwa uwanjani uchume utajiri halafu uachane na mchezo wenyewe ukiwa una uwezo wa kiuchumi.
Mchezo wa soka ni moja kati ya ajira za muda mfupi zaidi duniani. Mchezaji akicheza soka kufikia umri wa miaka 30 anaitwa mzee. Kumbuka kuwa licha ya kuwa na umri huo bado anakuwa amebakiza miaka 11 mbele ya kuruhusiwa kugombea Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Kwa dunia ya mtaani miaka 30 bado kijana sana, kwa dunia ya soka miaka 30 ni mzee sana.
Kila nikimtazama Ajib anapocheza soka nahisi ni kama vile namtazama mchezaji ambaye nje ya uwanja ana kazi nyingine anazoweza kufanya kama vile kuwa Ofisa Benki, Mkuu wa Kitengo cha TRA au mfanyabiashara ambaye mambo yake yapo safi. Haonekani kuupania sana mpira. Anaudharau.
Hata hivyo, majuzi nikawasikia baadhi ya watu wa Simba wakidai kwamba, Ajib na baadhi ya wachezaji wa zamani wa Simba wanakerwa na sifa nyingi wanazopewa wachezaji wapya wa Simba ambao wanaonekana kama vile wamekuja kuiondoa Simba katika utumwa wa miaka minne dhidi ya Yanga na Azam.
Nimesikia kwamba wachezaji wa zamani wanaamini kuwa viongozi wa Simba wanawajali zaidi wachezaji wapya. Inadaiwa kuwa hata pasi huwa hawawapi wachezaji wapya. Hili lilinishangaza kidogo. Kwa mchezaji mwenye kipaji cha Ajib sio mchezaji wa kujali mchezaji anayeingia au anayetoka katika Simba.
Kipaji chake kinajisimamia mwenyewe. Kama angekaza sasa hivi angekuwa kule ambapo Mbwana Samatta yupo. Lakini hata hapa alipo bado angeweza kuwa mchezaji wa kuhusudiwa kuliko wachezaji wenzake wa ndani au wale wa kigeni.
Mfumo wa kupokezana vijiti vya ustaa wa Simba kwa sasa ulipaswa kumwangukia zaidi Ajib. Katika miaka ya karibuni alianza kutawala Mussa Hassan Mgosi. Baadaye ufalme ukamuwangukia Mbwana Samatta ambaye alikuja kununuliwa na TP Mazembe.
Baadaye Ufalme ukamwangukia Emmanuel Okwi ambaye mpaka leo ingawa yupo Ulaya lakini bado mashabiki wa Simba wanamhusudu. Wachezaji hawa watatu wote, Mgosi, Samatta na Okwi waliwahi kucheza Simba. Wakapokezana ufalme kadri nafasi zilivyojitokeza.
Baada ya Okwi kuondoka, Simba haina Mfalme na ndio maana mashabiki wa Simba wanamkumbuka sana Okwi. Kwa nini wasimkumbuke sana Samatta? Ni kwa sababu nafasi yake ilizibwa vyema na Okwi.
Baada ya Okwi, mchezaji mwenye kipaji maridhawa ambaye alipaswa kuchukua nafasi ya ufalme ni Ajib. Hii ni bila ya kujali wachezaji wanaoingia au kuondoka Simba. Ajib bado hakuweza kuitumia nafasi hii vizuri.
Nadhani angeweza kufanya zaidi. Kwa chochote kizuri anachoonyesha, bado naamini kuwa anacheza soka kwa asilimia 50 tu ya uwezo wake. Kama angeweza kucheza zaidi ya asilimia hizo, hakuna mchezaji mwenye kipaji zaidi kwa sasa katika safu ya ushambuliaji kama Ajib.
Muda wa kujirekebisha bado anao mwingi. Hata kama siyo kwa kwenda kucheza na kutamba Ulaya, lakini bado ana muda mwingi wa kuwateka mashabiki wa Simba kama kina Okwi walivyofanya. Ajitume na kucheza soka kama vile anatoka uswahilini.
Kwa sasa nikimtazama Ajib na kipaji chake kikubwa na masikhara mengi huwa namchukulia kama vile ni mchezaji, ambaye ni mtoto wa mwisho katika familia moja ya kitajiri sana pale Masaki.
Huwa natabasamu sana jinsi anavyoudharau mpira.  Ni fundi sana, lakini angeweza kufanya zaidi na zaidi. Kipaji alichopewa ni adimu sana.