Zinatamba na ndinga kali ligi kuu Tanzania

Muktasari:

Gari kali na ya kisasa zaidi VPL iko pale Chamazi ambapo inamilikiwa na klabu ya Azam. Basi hilo ni aina ya Higer kutoka China. Basi hilo lina huduma zote ndani ikiwemo choo, TV katika kila siti, kiyoyozi na sehemu za kuchajia simu. Maisha yanahitaji nini tena?


TIMU za Jeshi ndizo zenye magari yanayofanana Ligi Kuu Bara, magari fulani hivi magumu na ya kijeshi ambayo yanatoka katika Kampuni za Ashok Leyland ya India.Ni gari za kijeshi na hazina starehe yoyote. Wanajeshi na starehe wapi na wapi? Ndio maana wanatumia ndinga hizo ngumu ambazo hutumika pia kwenye shughuli nyingine nyingine za kijeshi.  Pia, kuna timu nyingine za ligi hiyo, baadhi zinatumia magari ya kukodi huku wengine waliojikomboa kidogo wakitumia mabasi madogo aina ya Toyota Coaster. Ni gari chache tu ambazo ni kali. Mwanaspoti inakuletea orodha ya timu za Ligi Kuu ambazo zinatumia ndinga za maana katika safari zake, ndani ya miji yao ama pindi zinapokwenda kucheza mechi za ugenini katika mikoa mingine.


AZAM, HIGER

Gari kali na ya kisasa zaidi VPL iko pale Chamazi ambapo inamilikiwa na klabu ya Azam. Basi hilo ni aina ya Higer kutoka China. Basi hilo lina huduma zote ndani ikiwemo choo, TV katika kila siti, kiyoyozi na sehemu za kuchajia simu. Maisha yanahitaji nini tena?

Wachezaji wa Azam wanaweza kusafiri kutoka Dar es Salaam hadi Mbeya bila kushuka ndani ya gari kwani huduma zote zinapatikana hasa pindi wakiamua kusafiri na vyakula vyao huwa raha mustarehe. 

Kwa hapa nchini mabasi la kiwango cha Azam yapo machache ambapo moja linaenda Dodoma, lingine Tanga, Moshi na Arusha. Ukienda pale Ubungo utaona zimeandikwa pembeni ‘Gari la Daraja la Juu’ yaani Luxury Bus.

Hata hivyo pamoja na kuwa na ndinga hiyo kali Azam imekuwa ikitumia usafiri wa anga pindi inapoenda kucheza mechi zake za mbali kama jijini Mbeya, Shinyanga na Mwanza. Basi hilo limekuwa likibeba mashabiki na kuwahi katika mji husika ili kuwapokea wachezaji.


MBEYA CITY, MITSUBISHI

Unashangaa nini sasa? Mbeya City ndiyo timu ya pili VPL kuwa na ndinga ya maana. Ni gari aina ya Mitsubishi kutoka Kampuni ya Mitsubishi Motors ya Marekani ambayo pia ina matawi katika nchi mbalimbali duniani ikiwemo Thailand.

Mbeya City ilipewa gari hilo na mdhamini wao ambaye ni Kampuni ya BinSlum kupitia bidhaa zake za RB Battery jambo ambalo limeifanya gari hilo kuwa miongoni mwa ndinga kali VPL.

Ndani ya gari hilo kuna sehemu ya kunywea chai pamoja na eneo la kufanyia mikutano midogo. Ikitokea viongozi wa Mbeya City wanataka kuteta jambo lolote wakati wa safari wanaweza kuitana katika eneo hilo na kuzungumza yote.


YANGA, YUTONG

Klabu kongwe zaidi nchini, Yanga nayo imo miongoni mwa timu chache za VPL ambazo zinamiliki ndinga kali. Yanga inamiliki basi aina ya Yutong ambalo ilipewa na waliokuwa wadhamini wao Kampuni ya Bia ya TBL kupitia kinywaji chao cha Kilimanjaro.

Basi hilo ni la Daraja la Kati na viti vyake vinaruhusu kusafiri safari ndefu bila kuchoka sana. Basi hilo ni kama tu haya mabasi mengi yanayosafirisha abiria kwenda mikoani. Hapo Ubungo yapo mengi tu.

Hata hivyo, Yanga imekuwa ikitumia pia usafiri wa anga kwa safari zake za mbali kwa hofu ya kuwachosha nyota wake ambao ndiyo ghali zaidi nchini.


SIMBA, YUTONG

Kama ilivyo kwa watani zao Yanga, Simba nayo inamiliki basi aina ya Yutong ambalo pia ilipewa na TBL. Basi hilo ni la kisasa pia na siti zake zinaruhusu wachezaji kwenda safari ndefu bila kuchoka sana.

Hata hivyo, basi hilo halina huduma za kisasa kama ilivyo kwa ile ya Mbeya City ama Azam kwani ni zile Yutong za mwanzo ambazo hazikuwekwa mbwebwe sana.


MTIBWA, MINI-YUTONG

Mtibwa Sugar inamiliki basi flani hivi dogo aina ya Mini-Yutong kutoka China. Ni basi la muundo wa Yutong kubwa, lakini hilo lina uwezo wa kubeba abiria wachache. Gari hilo pia lina siti nzuri ambazo hazichoshi sana hata kwa safari ndefu jambo ambalo linawafanya nyota wa Mtibwa Sugar angalau kuweza kuwa na utulivu katika safari zao.