Kinachochelewesha dili la Pogba ni cha juu kwa wakala

Muktasari:

Juventus ambayo juzi Jumamosi ilifikia makubaliano ya kumsajili mshambuliaji Gonzalo Higuain kwa ada ya Pauni 78 milioni, ilisema haipo tayari kulipa cha juu anachotaka kulipwa Raiola, kiasi cha asilimia 20 hivyo kama Man United wanataka dili hilo likamilike, itabidi wao wamlipe wakala huyo.

KINACHOCHELEWESHA dili la Paul Pogba kukamilika klabuni Manchester United imetajwa kuwa ni cha juu anachotaka kulipwa wakala wake, Mino Raiola.

Imeelezwa kwamba Man United imeamua kuvutavuta kidogo kuhusu kukamilisha dili la uhamisho wa mchezaji huyo, ambaye ataweka rekodi mpya duniani kama uhamisho huo utafanyika. Man United na Juventus zimeripotiwa kukubaliana ada ya Pauni 105 milioni, kiasi ambacho hakijawahi kutokea katika historia ya uhamisho wa wachezaji duniani.

Imeelezwa kwamba wakala Raiola, ambaye ameamua kupanda ndege kwenda Miami, Marekani kujadili ishu za mwisho na Pogba kabla ya kuthibitisha uhamisho huo anataka alipwe cha juu kiasi cha Pauni 18.4 milioni, pesa ambayo Juve walisema wao hawapo tayari kumlipa wakala huyo labda kama tu Man United watamlipa wao.

Juventus ambayo juzi Jumamosi ilifikia makubaliano ya kumsajili mshambuliaji Gonzalo Higuain kwa ada ya Pauni 78 milioni, ilisema haipo tayari kulipa cha juu anachotaka kulipwa Raiola, kiasi cha asilimia 20 hivyo kama Man United wanataka dili hilo likamilike, itabidi wao wamlipe wakala huyo.

Raiola alikula cha juu alipomhamisha Poga kwenda Juventus mwaka 2012, alivuta tena pesa wakati kiungo huyo wa Kifaransa aliposaini mkataba mpya na miamba hiyo ya Turin na sasa anawataka Juve wampe asilimia 20 ya mkwanja ambao, watavuta kama cha juu chake, jambo ambalo Juventus wamefichua hawaoni kama Pogba ana thamani hiyo labda kama tu Man United watamlipa wakala huyo.