Temeke Market ndivyo hivyo haoo fainali

Muktasari:

Dalili za mapema ziliashiria Market kuibuka na ushindi baada ya kupata bao katika muda wa kawaida, lakini mwamuzi alilikataa kwa madai ya mfungaji, Nassor Kapama alikuwa amezidi, lakini ilipokuja hatua na penalti kilaini ikapenya fainali.


HABARI ndio hiyo. Temeke Market haoo fainali kama vipi we jiandae kukutanano nao Jumamosi wakati michuano ya Sports Extra Ndondo Cup 2016 itakapofikia tamati na bingwa wake kufahamika.

Market imefuzu hatua hiyo baada ya juzi Jumamosi kuikwanyua Makumba FC kwa mikwaju ya penalti 3-1 katika mechi kali iliyoshuhudiwa dakika 90 zikiisha bila timu kuona lango la mwenzake.

Katika pambano hilo, Makumba licha ya kupewa sapoti na nyota kadhaa wa Ligi Kuu akiwa Shaaban Kado aliyekuwa akiwanoa makipa wa timu hiyo, lakini Market ilikaza na kufanikiwa kutinga fainali ikiwa ni mara yao ya kwanza.

Dalili za mapema ziliashiria Market kuibuka na ushindi baada ya kupata bao katika muda wa kawaida, lakini mwamuzi alilikataa kwa madai ya mfungaji, Nassor Kapama alikuwa amezidi, lakini ilipokuja hatua na penalti kilaini ikapenya fainali.

Timu hiyo ilikuwa ikisubiri kujua itacheza na nani kati ya FC Kauzu na Misosi ambazo jana Jumapili jioni zilikuwa zikikwaruzana kwenye Uwanja wa Bandari.


Ushindi una raha yake.

Asikuambie mtu ushindi una raha yake bwana, baada ya kuhakikisha timu yao imetinga fainali, mashabiki na wachezaji wa Market waliangusha shangwe za kufa mtu na kuifunika bendi ya Makumba iliyokuwa imejaa wanenguaji wa kike.

Beki wa kushoto wa Market, Adeyum Saleh ndiye aliyepiga mkwaju wa mwisho na kuweka kimiani ndipo nderemo na vifijo za mashabiki hao wa Temeke zilipoanza kwa kushangilia ushindi huo.

Rais wa Market, Ahmad Ally amesema kwa sasa nguvu zao zote wanazielekeza kwa mpinzani anayekuja mbele yao kama ni majirani zao wa FC Kauzu ama Misosi ya Tandale.

Kumbe Kisiga anakubalika Kweli

Shaaban Kisiga mmoja ya waliofunga penalti iliyoibeba Marketi alishangiliwa mno na mashabiki na yeye alisema kwa ufupi;

“Najisikia furaha kuona nakubalika hadi huku kwa jumla nimefurahi kulivusha chama langu fainali, tunawashukuru mashabiki wote kwa sapoti yao.”