Kocha wa Azam, kujifunza Kiingereza

Muktasari:

Ili kuonyesha amedhamiria kuipeleka Azam mbali kocha huyo alisema hataangalia muda wa mchezaji amekaa na timu kiasi gani kama hataweza kumshawishi.

KOCHA mpya wa Azam, Mhispania, Zeben Hernandez, amesema amepeleka ombi kwa uongozi wa timu hiyo ili aingie darasani kujifunza Kiingereza. Hernandez anatumia lugha ya Kispaniola ambapo anakuwa na mkalimali anayefafanua kwa Kiswahili.

Alisema ingawa bado hajapata changamoto ya kulalamikiwa bado anaona muhimu kujifunza Kiingereza.

“Sijapata malalamiko hadi sasa kwa sababu lugha ya mpira ni moja,  lakini tayari tumeomba tujifunze pamoja na wachezaji ambao hawajui lugha hiyo ili kuweka wepesi zaidi ya wao kunifuata au kama kuna shinda ya kukutana nami moja kwa moja,” alisema.

Mbali na lugha pia alisema amepeleka ombi la kubadili baadhi ya vyakula vya wachezaji ingawa hakuweza kuweka wazi ni aina gani viachwe na kuongezwa.

“Wanavyotumia si vibaya sana ila nimeomba pia kama kutakuwa na uwezekano vibadilishwe baadhi,” alisema.

Ili kuonyesha amedhamiria kuipeleka Azam mbali kocha huyo alisema hataangalia muda wa mchezaji amekaa na timu kiasi gani kama hataweza kumshawishi.