Omog aanza mikwara ya JPM

Muktasari:

Kocha wao huyo aliliambia Mwanaspoti: “Siku ya Jumapili ilikuwa maalumu na mwanzo wetu wa kuanza ngwe nyingine ya maandalizi yetu kuanzia Jumatatu kwa sababu kuna mambo yatabadilika katika mazoezi yetu ambapo sasa tutafanya ufundi zaidi na fiziki itakuwa kidogo. Tulipoanza ilikuwa ni fiziki zaidi na ufundi kidogo.”


RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, John Pombe Magufuli (JPM) amekuwa akitekeleza asilimia 99.9 ya mambo anayoahidi, lakini mara kadhaa misemo yake imekuwa ikiwafurahisha hata wapinzani kumsikiliza na baadhi kudhani kwamba ni mikwara.

Mikwara hiyo ndio ambayo Kocha Mkuu wa Simba, Joseph Omog amewachimba wachezaji wake juzi Jumamosi na jana Jumapili na kuwaambia anataka nidhamu ndani na nje ya uwanja, atakayekwenda tofauti na yeye wasilaumiane.

Kocha wao huyo aliliambia Mwanaspoti: “Siku ya Jumapili ilikuwa maalumu na mwanzo wetu wa kuanza ngwe nyingine ya maandalizi yetu kuanzia Jumatatu kwa sababu kuna mambo yatabadilika katika mazoezi yetu ambapo sasa tutafanya ufundi zaidi na fiziki itakuwa kidogo. Tulipoanza ilikuwa ni fiziki zaidi na ufundi kidogo.”

“Ni kama darasa la vitendo, kuelekezana namna tutakavyocheza mechi zetu, mabeki wa pembeni wacheze vipi, wa kati watakuwa na majukumu yapi, viungo watafanya nini na washambuliaji pia watajua wanachotakiwa kufanya.

“Nataka kila mchezaji atambue majukumu yake kwa sababu uwezo wa kila mmoja katika kupokea, kutoa pasi nimeuona, wanavyocheza kitimu lakini sasa ni mbinu zenyewe na baada ya hapo, tutaanza kucheza mechi za kirafiki,”alisema Omog na kuweka wazi kuwa kwa sasa, wataendelea kutumia mfumo wa 4-2-3-1 kama wa msimu uliopita na baadaye ndiyo atajua cha kufanya na kuongeza.

“Mbali na hilo, nataka kila mmoja atambue nidhamu na ushirikiano mchezoni ndiyo siri ya mafanikio. Watambue kuwa Simba hakuna mchezaji bosi au staa, klabu ya Simba ndiyo bosi na kila mtu atafanya kazi yake kwa kufuata maelekezo ndani ya mchezo na nje ya mchezo.”

“Ninachokifanya ni kuandaa timu ya ubingwa wa Ligi Kuu Bara na siyo vingine na imani yangu tutafanikiwa, kikubwa ni umakini na kasi tuliyonayo iendelee hivyo,”alisema Omog.

“Naijua Ligi ya Tanzania na ushindani uliopo kwamba kuna Yanga na Azam, mimi sina habari nao na wala siwahofii wao, ndiyo maana kazi yangu kubwa ni kutengeneza timu yangu ya ushindi, halafu tukutane uwanjani.

“Kweli nimesikia juu ya kejeli, ninachopenda kusema, kikubwa ni kushirikiana tu ili mambo yetu yafanikiwe,”alisisitiza Omog kwa kujiamini pamoja na msaidizi wake, Jackson Mayanja raia wa Uganda, wanaamini kikosi hicho, kitazaliwa upya na kupata matokeo mazuri.


BADO STRAIKA TU

Simba inapokea mastraika wawili mmoja kutoka Ghana na mwingine Burundi muda wowote. “Mpaka sasa nafikiri kila sehemu ina matokeo mazuri ambako sijaridhika ni upande wa ushambuliaji tu, bado nahitaji straika mwingine mwenye uwezo wa kufunga mabao ya aina yoyote,”alisema Omog.

“Nafikiri, wiki hii kuanzia Jumatatu, nategemea kuna wachezaji kutoka Ghana na Burundi watakuja kwa majaribio,”alisema Omog na kufafanua straika huyo wa Burundi si Mavugo.


POLISI MORO

“Kama nilivyosema awali, wachezaji wa kigeni ni lazima waonyeshe utofauti na wazawa na siyo wawe watu wa kukaa benchi tu. Maamuzi ya kuwapitisha na kuwakata hawa waliobaki kipimo chao ni mechi za kirafiki, tutakapoanza hiyo Jumanne dhidi ya Polisi Moro,”alisema.